CHUO CHA BIBLIAherbhodges.com/books/TallyHoTranslations/Tally Ho the Fox... · Web viewShetani...

434
[Front Cover] MBWEHA TALLY HO! Msingi Kwa Ajili Ya Kujenga Wanafunzi Wa Yesu Wanaojiongeza Na Wenye Maono Ya Kuigusa Dunia Nzima Kimeandikwa Na Herb Hodges

Transcript of CHUO CHA BIBLIAherbhodges.com/books/TallyHoTranslations/Tally Ho the Fox... · Web viewShetani...

CHUO CHA BIBLIA

[Front Cover]

MBWEHA

TALLY HO!

Msingi Kwa Ajili Ya Kujenga

Wanafunzi Wa Yesu

Wanaojiongeza Na Wenye Maono

Ya Kuigusa Dunia Nzima

Kimeandikwa Na

Herb Hodges

Kimefasiriwa Na

Mch. Simon Joel Vomo

[Back Cover]

Herb Hodges aliyezaliwa na kukulia jimbo la Arkansas Marekani, aliokoka siku alipotimiza miaka kumi na nane, na akaitwa kuwa mhubiri muda mfupi baada ya hapo.

Ndugu Hodges alisoma katika Chuo Kikuu cha Biblia kiitwacho Southwestern Seminary huko Fort Worth Texas, na kuhitimu shahada ya Masters of Divinity mwaka wa 1962. Alichunga makanisa kwa miaka 27 katika majimbo ya Arkansas, Texas na Tennessee. Mwaka wa 1980, Ndugu huyu akawa mwinjilisti, mwenye kufanya mikutano ya uamsho, makongamano ya Biblia, makongamano ya Maisha ya Kiroho na Ufuasi. Huduma hii imemfanya atembelee karibu majimbo yote hamsini ya Marekani.

Amesafiri sana katika nchi za nje kwa ajili ya kufundisha wachungaji na viongozi kuhusu mkakati wa kujenga wanafunzi wa Yesu wanaojiongeza na wenye maono ya kuigusa dunia nzima katika kutimiza Agizo Kuu la Kristo. Amefanya safari kwa ajili ya kusudi hilo katika nchi za nje ni zaidi ya 70.

Ndugu Hodges na Judy mkewe wanakaa mjini Memphis, jimbo la Tennessee.

ORODHA YA YALIYOMO

ivUtangulizi

viiShukrani

1Sura Ya 1

1Maono Ni Muhimu Kiasi Gani?

34Sura Ya 2

34Agizo Lenye Kuamua Wajibu Wetu

85Sura Ya 3

85Wazo Lenye Kuamua Njia Tutakayotumia

104Sura Ya 4

104Ufunguo Ulioko Mlangoni Mwa Historia Ya Kanisa

133Sura Ya 5

133Vinavyotakiwa Ili Kufanya Wanafunzi

133Dawa Ya Daktari Kutibu Tatizo La Kuacha Agizo Kuu

158Sura Ya 6

158Mpango Wa Mungu Wa Kuongeza

177Sura Ya 7

177Hekima Ya Mkakati Wa Yesu

197Sura Ya 8

197Jinsi Kiwango Hiki Kifanyavyo Kazi Kanisani

219Sura Ya 9

219Maneno Yake Ya Mwisho, Wosia Wake

241Sura Ya 10

241Mbweha Tally Ho!

241Maana Ya Jina La Kitabu

253Kumalizia

253Maisha Ya Mbwa Wa Mwituni

264Muhtasari Wa Kila Sura

270Maswali Na Mapendekezo Kwa Ajili Ya Kujifunza Hiki Kitabu

Utangulizi

Kanisa la kawaida mahali popote lina kundi kubwa la “watendaji” wasiotumiwa ndani ya washirika wake. Mkristo wa kawaida hana kazi kulingana na viwango vya Kristo vya ajira, na yule Mkristo wa kawaida ambaye ana ajira, mara nyingi “hana kazi ya kutosha”. Basi anatumia muda mwingi na juhudi nyingi katika shughuli zenye kutoa matokeo madogo sana kwa habari ya kuwafikia na kuwajenga watu. Kanisa la kawaida la Kikristo hukutana Jumapili kwa Jumapili katika “jengo” na washirika wake ni “wasikilizaji” binafsi, ambao ni sehemu ya “wasikilizaji” wengine. Kwa kifupi ni kwamba, kanisa la kawaida limejaa “walioketi” ambao kusudi lao pekee ni kuja kanisani, kusikiliza mahubiri na kuondoka, wakitazamia kwamba mpango huo utasaidia katika kufikisha roho zao mbinguni kwa namna fulani na kuwawezesha kuwa na maisha mazuri kabla ya kufika huko. Kufanana kwa maisha hayo na maisha ya Kikristo yanayo-onekana katika Agano Jipya ni kwa bahati tu.

Ni dhahiri kwamba sisi Wakristo lazima tujifunze tena Agano Jipya, ambalo ndicho kitabu chetu cha kuongoza utendaji, na tujilazimishe kuona mambo kama yalivyo wakati tunapofanya hivyo. Lazima tujitangaze kuwa huru kutokana na mapokeo na desturi, na tugundue Agano Jipya linatuambia nini juu yetu sisi wenyewe, na kazi ambayo tumepewa na Mungu.

Mwandishi maarufu aitwaye Charles Swindoll aliandika hivi: “Hakuna kundi katika historia lililojithibitisha kuwa na uwezo katika utendaji kama ile timu ya uinjilisti ya karne ya kwanza – wale watu waliokuwa karibu sana na Kristo.” Huo ni ukweli usiokanika. Kwa nini? Bila shaka kilichochangia sana ni utaratibu ule ambao Yesu aliutumia katika kuwafundisha. Utaratibu huo umejengwa juu ya neno kubwa sana – “mwanafunzi”. Neno hilo linaonekana kwa nguvu sana katika vitabu vitano vya kwanza vya Agano Jipya, likitokea mara 269 (katika Injili ya Mathayo hadi Kitabu cha Matendo). Linatumika kama jina na tendo. Tena, linapotumika kama tendo, neno lenyewe ndilo amri pekee katika Agizo Kuu ambalo Yesu aliwapa wanafunzi Wake. Alisema hivi, “Wafanyeni watu kuwa wanafunzi”. Sasa, kwa uhalisi wa makundi makubwa ya waamini wasioendelezwa katika kanisa la leo (tena wengi wao wako kanisani kila tunapokutana), ni halali kwetu kuendelea kusema kwamba tumelifafanua vizuri neno ‘mwanafunzi’? Au kwamba sisi tumeelewa ipasavyo maana (au utaratibu) ya “kuwafanya watu kuwa wanafunzi”? Kwa uhalisi wa kanisa kutokuwa na mguso mkubwa kwa ujumla, pamoja na mabilioni ya watu ambao hawafikiwi na Injili duniani siku hizi, tunaweza kweli kuendelea kuamini kwamba tunatimiza Agizo Kuu? Sidhani.

Kurasa hizi ni mtazamo mpya na juhudi mpya za kutafsiri kwa kifupi sana kwamba sisi ni nani kama waamini wa Kristo, na kazi yetu kama wafuasi Wake. Ni maombi yangu kwamba Mungu atatusumbua na kutuamsha kupitia kurasa hizi kuwa na mtazamo mpya, kutaka kujihusisha kwa upya, na kuwa na matokeo mapya katika kutimiza Agizo Kuu la Bwana wetu.

Ninawiwa na marafiki wengi sana na waandishi wasio na idadi – wa kawaida na wa kanisa – kwa ajili ya mawazo tele na mbinu ambazo zimefupishwa na kuandikwa hapa. Pia, ninawiwa na wengi ambao wamenitia moyo kuandika vitu hivi, na wachache ambao wamenisaidia kufanya hivyo. Ushawishi wao ninauacha mpaka tutakapofika kwenye Kiti cha Hukumu cha Kristo, ambapo utatathminiwa kwa ubora sana na kupewa thawabu nzuri na bora kuliko niwezayo kuitoa mimi.

Herb Hodges - Mwandishi

Shukrani

Haiwezekani hata kuzaliwa kama mwanadamu bila kudaiwa sana. Kila mwanadamu anapozaliwa anakuwa na deni la pango la miezi tisa huko alikokuwa anakaa!

Kati ya wote wenye madeni, mimi ni mmoja mwenye kudaiwa sana, japo si kifedha. Watu wengi sana – walio hai na walikwisha pumzika – wamechangia faida nyingi sana maishani mwangu – hata siwezi kutaja yote. Ukweli ni kwamba siwezi hata kulipia riba ya kile walichowekeza kwangu.

Kwa habari ya kijitabu hiki, ninawiwa sana na makundi ya waandishi walioandika mawazo yao na kuhakikisha kwamba nimeyapata. Ninawiwa na wahubiri, waalimu na wenzangu ambao wametia kweli nyingi katika akili zangu, katika kipindi chote cha Ukristo wangu. Ninawiwa na watu kama Dom Fosco, ambaye kwa uvumilivu na uangalifu sana alihariri na kupanga upya kurasa hizi mara kadhaa; na Clint Davis, aliyeandika sura inayohusu Utangulizi wa Injili ya Luka (akitumia maandishi niliyotoa pamoja na kanda). Zaidi, ninawiwa sana kwa mke wangu mpenzi Judy, anayehudumia vile vile kama msaidizi wangu na mwandishi wangu, kwa sababu ya kunipenda na kuniunga mkono kwa hali yake tulivu, na kwa kuongezea hekima yake kubwa katika yangu ndogo niliyo nayo.

Ninawathamini na kuwaheshimu na kuwashukuru hao na wengine wengi. Wamenibariki sana! Narudia kusema tena – wamenipa deni kubwa sana. Rafiki zangu, asanteni mno. Herb Hodges

Sura Ya 1

Maono Ni Muhimu Kiasi Gani?

“Mahali ambapo hakuna maono, watu huangamia.”

Mithali 29:18

Katika lugha ya kiroho, “mtazamo wa KiMungu”, “hekima”, “uwezo wa kuona”, “kuangaziwa” na “maono” ni maneno yanayofanana kwa kiasi fulani. Maandiko mengi katika Neno la Mungu hudhihirisha umuhimu wa maono kama hayo. Tunasoma hivi katika Zaburi 119:18, “Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika Sheria Yako”. Na katika Zaburi 119:130 tunasoma hivi, “Kufafanusha maneno yako kuwatia nuru, na kumfahamisha mjinga.” Katika Yakobo 1:5 tunaambiwa hivi, “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu”. Katika Waefeso 1:15-19 – pamoja na mantiki yake – Paulo ameandika mojawapo ya sala zake kuu. Ninaamini kwamba hii ndiyo sala muhimu zaidi ambayo mwanadamu anaweza kumwombea mwenzake. Ni maombi ya “kuangaziwa”, kitu kimoja muhimu sana kwa ajili ya kuelewa mambo ya Mungu baada ya Kuzaliwa Mara Ya Pili. “Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuona”. Mambo mawili ya lazima kwa ajili ya ufahamu wa kiroho ni kuzaliwa upya na kuangaziwa.

Andiko kiongozi katika somo hili linatuonyesha kwa hali ya kinyume jinsi ambavyo “maono” ni muhimu. Kuona kwa mtu hutegemea “vioo” anavyotumia kuonea, kama ambavyo kusikia kwake kunavyotegemea “chujio” analotumia kusikiliza. Tunapoanza mafunzo haya kuhusu Agizo Kuu la Bwana Yesu kwa watu Wake, ni muhimu sana tuelewe thamani ya maono. Tunaambiwa na Mithali 29:18 kwamba, “Mahali ambapo hakuna maono, watu huangamia.” Huu ni mstari kamili: unafanya kazi kila mahali kwa ukamilifu kabisa.

WAZO LA KIROHO

Kwanza kabisa, fikiri kuhusu wazo la kiroho litolewalo hapa – wazo la “maono”. Likitazamwa katika mantiki yake, ni dhahiri kwamba maono yanayotajwa hapa ni ya aina pekee, maalum. Hapa kinachosemwa ni maono ya kiroho, ambayo ni maono ya maana sana mtu anayoweza kuwa nayo.

Kila kitu huanza kwa maono. Utakuwa kama unavyoona. Usichokiona huwezi kuwa. Utakuwa unachotazama, lakini usichokitazama, huwezi kuwa. Yaani, kile unachotazama kwa upendo sana, kwa kutamani, na kwa muda mrefu, ndivyo utakavyokuwa. Utakuwa kama kitu unachokitazama.

Hili jambo ni dhahiri katika dunia ya teknolojia ya vitu vya umeme siku hizi. Ukiacha picha fulani kwenye kioo cha kompyuta kwa muda mrefu sana, kitajiingiza mpaka katika mfumo mzima wa kompyuta na kuingia katika kila eneo na programu yoyote itakayotumika baada ya hapo. Kanuni hiyo ni halisi hata kwako: Kile unachotazama kwa muda mrefu sana kitaamua maisha yako.

Mkayun mmoja kutoka jimbo la Louisiana alikuwa anamwuza punda wake. Mtu mmoja aliyetaka kumnunua akamwuliza hivi: “Je, punda mwenyewe ana matatizo yoyote?” Yule Mkayun akajibu, “Haonekani vizuri” (japo kwa lugha yake alimaanisha haoni vizuri). Mnunuzi akasema, “Sijali sana kwa hilo. Je, anafanya kazi sana?” Akajibiwa, “Naam, ana bidii sana katika kazi, ila, haonekani vizuri tu” (kumbuka maana yake). Basi yule mtu akamnunua, na mwenye kumwuza akampandisha kwenye gari la huyo bwana mpya. Alipofika shambani kwake, alifungua nyuma ya gari lake na kumshusha yule punda. Mara, punda akagonga mti, halafu akajigonga kwenye zizi. Mkulima akapiga kelele kwa hasira, “Nimedanganywa! Huyu punda ni kipofu!” Akampakia punda kwenye gari, akamrudisha kwa mwenyewe na alipomfikisha, alipiga kelele na kusema, “Wewe ulinidanganya kuhusu huyu punda. Punda mwenyewe kipofu. Uliniambia uongo!” Yule mwuza punda akasema, “Hapana, sikukudanganya. Nilikwambia vizuri kabisa kwamba, ‘punda haonekani vizuri’!” (Bila shaka unakumbuka maana yake kwa kikwao.)

Ndugu Oswald Chambers ambaye ni mwandishi maarufu wa kitabu kiitwacho My Utmost For His Highest na vitabu vingine vizuri sana vya kujisomea kwa ajili ya kukua kiroho, aliandika kwa utambuzi mkubwa sana, kama ifuatavyo: “Ni rahisi zaidi kumtumikia Mungu bila maono. Ni rahisi kumfanyia Mungu kazi bila ya mwito. Kwa sababu, hapo husumbuliwi na yale Mungu anayotaka. Unaongozwa na akili za kawaida, ila juu yake unatia hisia za Kikristo. Lakini kama ukisikia agizo kamilifu la Yesu Kristo hata mara moja tu, ufahamu wa kile Mungu anachotaka kitakuwa lengo lako tangu wakati huo na kuendelea, nawe hutaweza kumtumikia kwa msingi wa akili zako za kawaida.” Hebu soma maneno hayo mara kadhaa kabla ya kuendelea mbele katika mafunzo haya. Nimetumia wino mwepesi kutilia mkazo.

Kuona kimwili ni muunganiko wa vidokezo vyenye kuonekana (yaani, kitu halisi katika dunia inayomzunguka mtu) na ujuzi pekee (jinsi mtu anavyotambua hivyo vidokezo vinavyo-onekana). Kidokezo chenye kuonekana kinaweza kisibadilike kamwe, lakini kikiisha onekana na kunasa kwenye macho ya mtu, kinaweza kupotoshwa, kukataliwa, au kupokelewa – yaani, kinategemea tafsiri ya mtu aliyekiona

Katika zile hisia tano za asili, kuona ni hisia mojawapo ambayo mtu hafai kupoteza. Ralph Sockman alikuwa sahihi aliposema hivi, “Jicho ndiyo askofu wa hisia”. Claud Monet, mchora picha maarufu wa Kifaransa alisema hivi, “Mimi ni mfungwa kamili wa macho yangu”. Kwa sehemu kubwa, hiyo ni kweli kwa kila mtu. Kuona (au kutambua) ndicho kiini cha kila kitu. Kanuni ifuatayo itakuwa kweli: Kuona hupelekea kwenye Hatua (au Utaratibu), na Hatua zitaongoza kwenye Matokeo. Ni dhahiri kwamba katika kanisa la Yesu Kristo tuna matatizo sana kwa habari ya matokeo. Ni kwamba hatutoi aina ya Wakristo waliosababisha Kitabu cha Matendo! Basi, kama tunachotoa kina upungufu, ni kwamba kuona kwetu kuna upungufu pia.

Maono ya kiroho ni kitu gani? Tafsiri moja ya Biblia kwa lugha rahisi inafafanua Wakolosai 1:9 kwa njia itakayotusaidia. Paulo aliandika hivi, “Ninaomba kwamba mwone mambo kwa mtazamo wa Mungu.” Maono ya kiroho ni kuona mambo kwa mtazamo wa Mungu. Lakini Biblia inatuambia wazi kwamba mtazamo Wake hautakubaliana na wa kwetu (ktk Isaya 55:10). Basi, ni muhimu kuwepo na urekebishwaji wa dhati kiroho ili tuweze kufikisha mtazamo wetu kwenye hali ya kukubaliana na mtazamo wa Mungu.

Ndugu Dawson Trotman, mtu mwenye maono makubwa kiroho, alisema hivi, “Maono ni kupata moyoni mwako kile kilicho moyoni mwa Mungu.” Lakini, Mungu ana nini moyoni Mwake? Mstari wetu kiongozi unajibu swali hilo kwa neno moja tu: “watu”. Moyoni mwa Mungu kuna watu. Watu wangapi? Watu wote. Moyoni mwa Mungu yuko kila mtu aliyeko duniani. Naye anatazamia watoto Wake kukubaliana Naye katika jambo hili linalomgusa sana.

Anatazamia sana kwamba watoto Wake wataigusa dunia nzima. Basi, utume wa dunia nzima unahitaji maono ya dunia nzima. Hii inamaanisha kwamba Wakristo wengi wanahitaji kufikishwa mahali ambapo wataanza kuona wajibu wao wa kuibeba dunia nzima ili waweze kuanza kuigusa kwa ajili ya Kristo.

Hebu fikiri tena swali hili: Je, moyoni mwa Mungu kuna nini? Je, kinachotakiwa kuwa kiini cha moyo wa kila aaminiye, na katika ndoto zake na maono yake ni nini? Mstari wetu unatoa jibu: watu. “Mahali ambapo hakuna maono, watu huangamia.” Basi, ni kwa nini kiasi cha 4 kwa 5 ya watu wa duniani ndiyo wamepelekewa Injili kwa udhaifu sana, na kufundishwa kwa udhaifu sana kuhusu yaliyomo katika Injili na mkakati wake, huku nusu ya binadamu hawajawahi kusikia jina la Yesu kwa kiwango cha kufikia ukombozi? Je, Ukristo uliofunuliwa katika Kitabu cha Matendo ungevumilia hali hii? Hapana kamwe! Basi, nini tofauti kati ya Ukristo wa Kitabu cha Matendo na Ukristo wa siku za leo, ulioko katika kanisa? Je, Yesu wa kanisa la leo ni tofauti na yule wa kanisa la kwanza? Hapana. Je, Roho Mtakatifu ni tofauti. Hapana. Je, Biblia ni tofauti? Ndiyo, lakini uzuri wa hili uko kwetu, si kwa Wakristo wa kwanza. Wao hata hawakuwa na Agano Jipya lililokamilika. Sisi tunalo, lakini pamoja na hilo, hatujafikia karibu na jinsi wao walivyoweza kuigusa dunia yao.

Basi, nini tofauti kati ya Ukristo uliosababisha Kitabu cha Matendo, na Ukristo wetu sisi? Pamoja na kwamba itaonekana kama nimerahisisha sana, mawazo yangu ni kwamba tofauti ya msingi kati ya “Ukristo wao” na “wetu” ni mkakati. Mkakati wao ulionyesha kutokujali kwao kujenga taasisi na kukazia zaidi kuwajenga watu. Mkakati wao ulikuwa wa kulipuka (kuelekea nje) badala ya kubomokea ndani. Yesu alifundisha watu kumi na mbili, “ambao aliwaita mitume” (ktk Luka 6:13). Kwa nini akawapa jina tofauti? Ni kitu gani kikubwa, ni kitu gani anachokazia, na anataka tuone nini wakati mtindo Wake mkuu (hata unaweza kusema, wa pekee) wa kufundisha uliwalenga watu kumi na mbili, na kuacha neno la kawaida la “mwanafunzi” na kuwapa jina tofauti na la kipekee sana la “Mtume”? Nadhani siri iko katika maana ya neno lenyewe. Ni neno la Kiyunani linalotokana na kuunganika kwa maneno mawili madogo. “Stolos” maana yake ni “kutuma”. “Apo” maana yake ni “mbali na.” Hapo ndipo penye siri. Aliwajenga hao watu maalum waliochaguliwa ili “kuwa pamoja Naye” (ktk Marko 3:14) kwa muda aliohitaji tu kuwafundisha na kuwaingizia uzima Wake, maono Yake, na mkakati Wake. Baada ya hapo, mpango Wake ulikuwa kuwatuma waende mbali na eneo lao la mafunzo kiasi ambacho wangeweza, au ingewezekana, au wangetaka kwenda. Mwongozo Wake ulikuwa: Kuingia ndani kwa muda, lakini Kutoka kikazi! Na ukweli kwamba orodha ya Zawadi (Watu Wenye Karama) alizotoa kwa Kanisa Lake inaanza kwa neno “mitume” (ktk Waefeso 4:11) unaonyesha kwamba mtume alitolewa kwa kanisa ili kuwafanya washirika na huduma ya kanisa kuelekea nje.

Imani yangu thabiti kabisa ni kwamba, Yesu Kristo anamtazamia kila mtu aliyeokoka atawaliwe na maono ambayo daima yanafanya macho yake na miguu yake kutoka nje – kwenda hadi miisho ya dunia. Ni kweli alitupa sisi utume wa dunia nzima, lakini lazima nirudie tena kwamba utume wa dunia nzima unahitaji maono ya dunia nzima. Pia ninaamini kwamba maono na shughuli yenyewe vinapaswa kuwa kitu binafsi, wala siyo kitu kinachofanywa kitaasisi. Mkristo wa kanisa la siku hizi “asiyefanya kitu”, asiyejihusisha katika kazi ya kugusa dunia nzima, hafikiriki na hawezi kuvumiliwa katika mpango wa Mungu. Ninaamini kwamba Yesu anamtazamia kila mtu aliyeokoka awe na maono na mkakati (ambao ulionyeshwa na Yeye Mwenyewe) wa kuigusa dunia nzima hadi miisho ya dunia na mpaka ukamilifu wa dahari!

Kumbuka kwamba Mungu anao watu wote katika moyo Wake, Naye anatazamia sisi pia tuwe hivyo. Henrietta Mears, mwalimu maarufu sana Mkristo, alisema hivi: “Ninapoitazama huduma yangu, nafikiria dunia nzima. Kingine chochote hakitamsahili Kristo wala mapenzi Yake kwa ajili ya maisha yangu.” Mkristo asiyekuwa na maono kama hayo ni kama chombo cha kusafiria katika anga za juu kilichopoteza ratiba yake ya safari. Mwendo kasi wake utakifanya kufika mahali, lakini lengo lake linaweza kufutwa kama kitakataa kufanya kazi kulingana na ratiba yake. Sisi kama Wakristo ratiba yetu siku zote ni ile yenye kulenga Kugusa Dunia Nzima, na mkakati wake maalum umetamka katika Agizo Kuu la Bwana wetu. Kitu chochote kinyume cha hicho kimetokana na mwanadamu, na hakimtoshelezi Mungu.

Ni kitu muhimu sana kutambua kwamba, Roho Mtakatifu aliposhuka siku ile ya Pentekoste katika uwezo mkamilifu wa ukombozi, tokeo la kwanza linalotajwa la kuja Kwake ni kwamba “vijana wenu wataona maono na wazee wenu wataota ndoto” (ktk Matendo 2:17). Mara nyingi hili limegeuzwa na kuonekana ni kitu cha kipekee na cha siri sana kiasi kwamba kimetengwa kwa ajili ya watu waonaji wasiokaa na watu. Sivyo. Ukweli ni kwamba hii inapaswa kuwa kawaida ya maisha kwa Wakristo wa kiroho. Kulingana na mantiki, hayo maono na ndoto si yale yanayotokea wakati watu wamelala, bali ni yale yanayopatikana na kujulikana na moyo uliojaa Roho Mtakatifu. Kwa mantiki hiyo, ndoto hizi na maono ni ndoto za mkakati pamoja na maono yatakayopelekea kwenye kufanya kikamilifu kabisa Agizo Kuu la Bwana wetu. Ndoto na maono ya mikakati aina hiyo vinatakiwa kuwa vitu vya kawaida na vya kila siku katika maisha ya Wakristo wa Agano Jipya wa kawaida, wala si mambo ya kiajabu na kushangaza yanatokea kwa watu fulani wachache wenye aina fulani ya maisha.

[USHUHUDA WA MWANDISHI – Nilikuwa nafundisha kwenye mkutano wa viongozi wa kanisa miaka kadhaa iliyopita. Nikapewa kisa hiki kifuatacho na ndugu asiyekuwa mchungaji. Alianza kwa kunionyesha jengo lenye ghorofa kumi na nne, kisha akasema kitu alichokuwa ameambiwa kuhusu wakuu wa shirika la hapo.

“Lile jengo ni makao ya shirika tajiri sana. Wakati fulani huko nyuma, viongozi kadhaa wa ngazi ya juu katika shirika hilo walimwendea kiongozi mkuu wakamwuliza, ‘Hivi huyo makamu wako wa kwanza ana nini juu yako kiasi kwamba inabidi aendelee kuwepo? Mbona unamlipa mshahara mkubwa kiasi hicho wakati hazalishi chochote?’ Yule mkuu alipowauliza maana yao, walimpeleka hadi ofisini kwa msaidizi wake huyo na kumwambia achungulie dirishani. Makamu wake alikuwa ameegama kwenye kiti chake kinachozunguka, na hakikuwa kinatazama mezani. Alikuwa ameweka mikono nyuma ya kichwa chake, na miguu ameiweka kwenye dirisha. Hakuwa anajigusa – pengine alikuwa kalala au alikuwa anachungulia nje. Wakamwambia, ‘Unaona tunachosema? Hiyo tu ndiyo kazi yake, lakini analipwa mshahara mzuri sana. Kwa nini?’ Yule mkuu wa shirika akajibu kwa upole sana, hivi: ‘Nisikilizeni kwa makini sana. Mwaka jana, huyo jamaa aliyeketi kwenye hicho kiti katika hiyo ofisi alipata wazo lililoletea shirika hili zaidi ya Dola milioni 85 za Marekani… Mwaka huu, ana kazi moja tu ….’!” MWISHO WA USHUHUDA]

Wapendwa waamini wenzangu, yuko wapi mtu katika kanisa la leo anayefikiri kuhusu wazo la Mungu la Dola milioni 85? Yuko wapi mtu anayeona maono ya Mungu ya Dola milioni 85, au mwenye kuota ndoto ya mkakati wa Mungu wa Dola milioni 85? Mungu Muumbaji wa Biblia hakosi mawazo makubwa ya kiumbaji, lakini, wako wapi watakatifu Wake wa kawaida kabisa ambao wanaona mkakati kwa mtazamo Wake, na kupata moyoni mwao yale ambayo Mungu anayo moyoni Mwake kimkakati?

Hebu nitaje kanuni nyingine inayohusu maono.

Hakuna maono = kushindwa kabisa;

Maono yenye mpaka = mafanikio kidogo;

Maono – mpango – matendo = ni ndoto tu;

Maono + mpango – matendo = ndoto yenye kutisha (kusikia hatia); ila

Maono + mpango + matendo = huduma ya kiroho yenye matokeo.

Ona kwamba kipimo cha maono ya mtu ni matendo yanayosababishwa na maono hayo. Pasipo matendo, wewe na vipawa ulivyo navyo mnabakia kwenye kiwango cha “kuwa na uwezo wa kufanya kitu”. Hali hiyo ni uwezo uliolala ambao haufanyiwi kazi kamwe kupitia maono.

Myles Munroe ambaye ni kiongozi Mkristo alisema hivi kuhusu uwezo wa mwamini kufanya kitu katika kitabu chake kiitwacho Understanding Your Potential: “Mahali penye utajiri sana hapa duniani si katika maeneo ya mafuta huko Kuwaiti, Iraki au Saudi Arabia. Wala si katika machimbo ya dhahabu na almasi huko Afrika Kusini, au machimbo ya uranium huko Urusi au katika machimbo ya shaba yaliyoko Bara Afrika. Utashangaa tu lakini, utajiri mkubwa sana katika dunia yetu uko mita chache tu kutoka nyumbani kwako. Uko katika makaburi yenu. Huko chini, kumezikwa ndoto ambazo hazikuwahi kutimizwa, nyimbo ambazo hazikuwahi kuimbwa, vitabu ambavyo havikuandikwa, picha ambazo hazikuchorwa, mawazo ambayo hayakutolewa, maono ambayo hayakufanyika uhalisi, vitu vilivyobuniwa ambavyo havikutengenezwa, mipango ambayo haikutoka kwenye mawazo ya mtu na makusudi ambayo hayakutimizwa. Makaburi yetu yamejaa uwezo wa kufanya vitu ambao haukufanikiwa.

“Uwezo wa kufanya vitu unadai kwamba usikubali kutosheka na kitu ulichofanikisha. Adui mmoja ambaye ni mkubwa sana wa uwezo wako kufanya vitu ni mafanikio. Mafanikio kidogo huharibu uwezekano mkubwa! Ili uweze kufikia uwezo wako kamili wa kufanya vitu, hutakiwi kutosheka na ulichofanikisha. Pia ni muhimu kwamba usiruhusu kile usichoweza kufanya kiingiliane na kile unachoweza kufanya. Janga kuu maishani si kifo, bali ni maisha ambayo hayakufikia kilele chake katika uwezo wa kufanya vitu.

“Katika kurahisisha dhana hii, hebu tutazame kitu kimoja katika uumbaji ambacho kina nguvu sana … mbegu. Nikishika mbegu mkononi na kuukuliza, ‘Nina nini mkononi?’ utasemaje? Pengine utajibu kilicho wazi kabisa … ni mbegu. Lakini, ukielewa asili ya mbegu, jibu lako linaweza kuwa uhalisi japo halitakuwa ukweli. Ukweli ni kwamba nimeshika msitu mkononi mwangu. Ni hivi: Katika kila mbegu kuna mti, na katika kila mti kuna matunda au maua yenye mbegu ndani yake. Na hizo mbegu nazo zina miti ambayo ina matunda yenye mbegu ndani yake … ambazo zina miti yenye matunda yenye mbegu, na kadhalika na kuendelea. Unachokiona hapa si yote. Kwa hiyo, tofauti kati ya mbegu moja na utoaji wa chakula kama vile ngano inayoweza kulisha dunia nzima ni kitu kinachoitwa ‘uwezo wa kufanya vitu.’ Hicho ndicho kiwango cha tofauti kati ya unachoona na kinachowezekana.

“Kama Musa angekufa kabla hajaona kile kichaka kilichokuwa kinawaka moto … au Paulo kabla ya kukutana na Yesu akiwa njiani kwenda Dameski … au Ibrahimu kabla ya Isaka kuzaliwa. Maandiko na historia vingekuwa tofauti sana. Kama Martin Luther angekufa bila ya kuandika yale matangazo yake … au Charles Wesley bila ya kutunga nyimbo zake … au John Wycliff bila kufasiri Biblia katika lugha ya Kiingereza. Historia ya Kanisa ingekuwa tofauti sana.

“Sijui ingekuwaje kama baba yako angekufa kabla hujatungwa mimba, au mama yako kabla hujazaliwa. Dunia ingepoteza nini kama usingezaliwa? Je, dunia itakosa nini kwa sababu unashindwa kuishi kufikia kiwango cha uwezo wako wote? Je, utakwenda kaburini na nyimbo, vitabu, magunduzi au dawa?” Mimi nimetumia wino mwepesi hapa kuweka msisitizo maneno ya mwandishi.

Je, inawezekana kwamba dhambi kuu ya Wakristo imo katika uwezo wao wa kufanya mambo ambao haujafikiwa? Tena, uwezo mkuu wa kufanya mambo ambao haujatumiwa katika siku za leo ni katika eneo la kutimizwa Agizo Kuu la Bwana wetu. Yeye amekupa wewe nafasi maalum katika Kuufikia Ulimwengu Kikamilifu, na ni nafasi kubwa kuliko yoyote uliyowahi kuwa nayo. Hii nafasi haiwezekani bila ya maono kwamba inawezekana. Basi, kitu muhimu kuliko vyote katika maisha yako ni kuwa na maono yanayokubaliana na Mungu, na kuyafuatilia. Kwa kuwa kazi uliyopewa inahusu dunia nzima, maono yako lazima yawe hivyo hivyo. Je, una maono ya aina hiyo?

Sasa – watu kama wewe na mimi – wenye ubinafsi, kujijali, wenye kujali kwao na wenye kujiona wanapataje maono ya Mungu? Angalia kanuni hii, inayoweza kufanya kazi: habari sahihi ukijumlisha na kuangaziwa kiroho vitaleta maono, ambayo yatasababisha motisha, na hiyo motisha itapelekea utendaji wa kiroho wenye matokeo. Hapo, ona kwamba maono huanza kwa kupata habari sahihi. Sawa na ambavyo kuona kimwili kunavyoanza kwa kuwepo kwa kivutio cha nje, ndivyo na maono kiroho yanavyoanza kwa ukweli wa Mungu katika Maandiko na kila kitu ambacho kinahusiana na Maandiko. “Matofali” ya kujengea maono hayo ni: kufahamu Maandiko kiasi cha kutosha na moyo sikivu wa kusikia Maandiko na kuyatii, halafu ufahamu wa jiografia ya dunia na tamaduni za nchi mbalimbali, utambuzi kiroho wa matukio, maombi, kujisomea ili kupata habari, ujuzi binafsi (“njoo uone” katika Maandiko) wa baadhi ya maeneo ya kimisheni duniani, ushirikiano na waamini wenye maono, kujitoa kwa ajili ya kutoa kuhusu mambo ya umisheni, kukutana na wamishenari na Wakristo wenye kugusa dunia, na maamuzi mbalimbali katika maisha. Unaweza kuanza kushirikiana na Mungu katika kujenga maono ya kiroho katika maisha yako leo. Lakini, ni dhahiri – na inasikitisha sana – kwamba Wakristo wengi unaoshirikiana nao mara kwa mara hawana maono kama hayo.

HALI YA KUSIKITISHA

Pili – fikiri kuhusu hali ya kusikitisha ambayo inatajwa hapa, kwamba, “Mahali pasipo na maono.” Neno “mahali” linaweza pia kutamkwa hivi: “popote”. Basi, haya ni maneno yanayohusu kila mahali. Kwa lugha ya KiBiblia, nini maana ya “pasipo maono”? Maana yake ni kwamba Mungu hatambuliwi, wala mpango Wake mkamilifu. Maana yake ni kwamba Shetani, “mungu wa dunia hii” ame”pofusha mawazo ya watu” wasione mambo ambayo ni ya muhimu na yenye maana! Hawawezi kuona wala kuyaelewa mambo haya bila ya kuzaliwa upya pamoja na kuangaziwa (ona 1Wakor. 2:9-14). Basi, hakuna mawasiliano ya kudumu baina ya mbingu na mioyo ya watu. Hakuna biashara na kile kisichoonekana, cha milele, cha kiroho, na ambacho ni halisi. Hakuna kumsikiliza Mungu na kumtazama Yeye. Kwa kifupi ni kwamba, “pasipo maono” maana yake ni kwamba watu hawamwoni “Aliye Juu na Mtakatifu, mwenye kutamalaki Milele.” Basi, tunakuwa na mipaka na kuona maeneo yetu madogo pamoja na upeo wetu, na mipango yetu midogo, ya kibinafsi, ya kidhambi tu. Mtu mwenye mipaka kiasi hicho, na mwenye mipango yenye mipaka kiasi hicho hatimaye anabomokea ndani yake mwenyewe. Ni hivi: Kila kitu huanza kwa maono ya kweli. Ona lile neno “kweli”. Ninalitumia kama kinyume cha kutokuwa na maono, maono bandia na maono yenye mipaka.

Lazima tukubali – kwa huzuni sana – kwamba, watu wengi walio-okoka wana ubinafsi, wanajipenda wenyewe na wametawaliwa na hali ya kujilinda kwa kiwango sawa na watu waliopotea tu. Yaani, wengi katika watu walio-okoka ni wenye dhambi (tafsiri “dhambi” kuwa ni ubinafsi) kama waliopotea tu. Kwa nini? Hapo tena, andiko letu la msingi linatoa jibu: Hakuna maono. Si mara nyingi tunaona mambo “kwa mtazamo wa Mungu”. Si mara nyingi mioyo yetu inakuwa na kile ambacho Mungu anacho moyoni Mwake – dunia nzima ya watu mmoja mmoja waliopotea.

Mtazamo ni muhimu sana. Kuona kwa mtu hutegemeana na aina ya vioo anavyotazamia, sawa na jinsi kusikia kwa mtu kunavyotegemeana na chujio analotumia kusikilizia. Hebu tutoe mfano wa kusaidia kueleweka kweli hiyo.

Mwaka wa 1877, mtaalamu wa nyota Mmarekani aliyeitwa Percival Lowell aliushangaza ulimwengu wa sayansi kwa kutoa wazo kwamba, kutokana na ushahidi aliokuwa amekusanya, kulikuwepo na dalili za uhai na viumbe wenye akili katika sayari ya Mars. Nadharia yake – kwa sehemu – ilitokana na yeye kuona vitu alivyoita “mifereji” kwenye sayari hiyo. Wanasayansi wakabebwa na tamko hilo kwa kishindo. Lakini, walikuwepo watu wachache ambao tangu mwanzo walikuwa wamefahamu kwamba hiyo sayari haina mifereji. Baadaye, Bwana Lowell alipata tatizo kubwa kiafya, lililoanza kujitokeza. Jopo la matabibu walimpima na kugundua tatizo lenyewe. Ugonjwa wake haukuwa umejulikana sana siku zile, basi wakauita jina lake – “Lowell’s Syndrome”. Ishara mojawapo ilikuwa kwamba, alipoketi muda mrefu akichunguza kitu fulani, sura na ukubwa wa mishipa ya kupitisha damu katika macho yake ilikuwa inaonekana kwenye hicho kitu alichokuwa anakichunguza. Basi, badala ya kuona “mifereji” kwenye sayari ya Mars kwa njia ya darubini, alichokuwa anakiona ni mishipa yake mwenyewe ya damu. “Alibeba” kile alichodhani anakiona, katika kichwa chake mwenyewe. Mtazamo!

Ufuatao ni mfano mwingine tena.

Dakta Harold Lindsell, mhariri mstaafu wa jarida liitwalo Christianity Today, alihudhuria kliniki ya macho ya Kijapani zamani kidogo. Akiwa darasani siku moja, mkufunzi aliinua chati kwa ghafula mbele ya darasa. Akauliza hivi: “Ni wangapi mnao-ona namba nane?” Lindsell peke yake ndiye aliinua mkono wakati huo. Alisema baadaye kwamba alidhani ni njama – kwamba darasa lote lilikuwa limekusudia kumcheza shere. Lakini, mkufunzi akauliza, “Ni wangapi mnaoweza kuona namba kumi na nne?” Kila mtu darasani aliinua mkono! Ndipo mwalimu akazungumza na Ndugu Lindsell na kumwambia, “Mheshimiwa! Kuna mtu ambaye amewahi kukwambia kwamba wewe una matatizo ya kuona rangi?” Ni kwamba hapakuwa na hila yoyote. Kila mtu siku hiyo katika lile darasa alikuwa anasema ukweli – kulingana na alivyouona. Mtu mmoja kweli aliona mamba nane huku wengine wote wakiona namba kumi na nne. Mtazamo huo!

Ni hivi: Mtazamo hufunika kila kitu ambacho hakihusiki, na kusababisha maono yatawaliwe na kile ambacho kinahusika. Kwa hiyo ni muhimu sana.

Mwanamke mmoja alisogea karibu na Dakta G. Campbell Morgan, mwalimu maarufu wa Biblia wa zamani. Akamwuliza huvi: “Hivi Dakta Morgan, unaamini kweli kwamba Mungu anajali mambo madogo madogo ya maishani mwetu?” Dakta Morgan akamjibu kwa upole sana, hivi: “Mama. Hivi kweli unaamini kwamba katika maisha yako kuna kitu kikubwa sana kwa Mungu?” Mtazamo huo.

Hayo ndiyo yanayofanywa na mtazamo. Yanaondolea mbali habari fulani au mambo fulani kuwa si ya maana, na kukuza mengine kuwa muhimu mpaka kufikia kiwango cha “kweli”. Lakini, mtazamo unaweza kutokana na mtazamaji mwenyewe kiasi cha kutokuwa halisi katika hali ya kawaida kabisa. Yaani, hata unaweza usitoe nafasi ya kitu halisi kabisa kilichopo kuonekana. Acha nikupe mfano wa KiBiblia kuhusu mtazamo.

Sura ya kumi na tatu ya kitabu cha Hesabu ni taarifa ya hadithi ya taifa la Israeli wakiwa Kadeshi Barnea, kusini kidogo tu ya nchi ambayo Mungu alikuwa amewaahidi. Bila shaka walikuwa tayari kuingia katika Nchi yenyewe. Lakini, walipatwa na hali ya kutokuamini, wakatuma kikundi cha wapelelezi kumi na mbili kwenda kutazama udhaifu wa nchi ile. Wapelelezi wake wakarudi na taarifa iliyogawanyika. Wote walikubaliana kwamba nchi ilikuwa inakaliwa na watu ambao hawakuwa na wazo la kuiachia. Halafu, wapelelezi kumi – idadi kubwa kabisa – wakapendekeza kwamba wasiiteke nchi kwa msingi kwamba wakazi waliokuwemo nchini “wana nguvu kuliko sisi,” na kwamba wana wa Israeli walionekana kama mapanzi, wakilinganishwa na majitu. Wapelelezi wawili walitosha ushauri “wa wachache”. Wakikiri ukweli ule ule, wao waliendelea na kusema hivi: “Hebu na tupande mara moja na kuitwaa nchi, kwa sababu tuna uwezo kabisa wa kuiteka” (ktk Hesabu 13:30). Ni hivi: Wale wachache walimwingiza Mungu katika uamuzi wao, kitu ambacho wale wengi hawakukifanya. Basi, mitazamo miwili ikaamua mashauri yale mawili yaliyotolewa: mtazamo mmoja ulimhusisha Mungu, ule wa pili haukufanya hivyo. Wote waliona “majitu”; wengi wao walijiona kuwa “mapanzi”. Wawili tu ndiyo walimwona Mungu. Au basi: wengi walimwona Mungu kupitia hao majitu, na hao wakaonekana kuwa wakubwa kuliko Mungu. Wale wachache waliwaona majitu kupitia Mungu, na Mungu akawa mkubwa kuliko majibu. Basi, mtazamo wao uliamua mapendekezo yao na utendaji wao. Hapo ndipo penye tofauti kati ya “maono” na “pasipo maono”!

Akili ya kibinadamu siku zote itakupa mtazamo wako kulingana na maoni yako. Muujiza tu wa kuangaziwa ndiyo utakaokupa mtazamo wa Mungu. Hapo ndipo kuna tofauti kati ya “pasipo maono” ambayo hatima yake ni “watu huangamia”, na “maono” ambayo kwa hiyo watu hustawi na kufanikiwa.

Jaribu kufikiri kutokuwepo na maono ya kiroho katika madhabahu ya kanisani unapoabudu. Huna haja ya kufikiri sana kama utatembelea makanisa mengi! 1Samweli 3:1 inasema, “Neno la Mungu lilikuwa adimu katika siku hizo. Hayakuwepo maono ya wazi (au, ya mara kwa mara).” Ukisoma historia ya taifa iliyotokana na wakati huo utagundua kwamba mambo ya kusikitisha sana yalitokea kwa sababu ya kutokuwepo na maono.

Ingekuwaje kama isingekuwepo Injili inayohubiriwa kutoka madhabahu ya kanisa unalohudhuria? Kutokuwepo kwa kutambua kwamba mtu amepotea pasipo Kristo? Kutokuwepo na kuamini nguvu zenye kubadili maisha za Roho Mtakatifu? Kutokuwepo kwa mafafanuzi ya ndani sana na wa milele wa mausia ya Mungu? Kutokuwepo kwa mafunuo ya hazina nyingi sana zisizomalizika zilizomo katika Neno la Mungu? Kutokuwawezesha wasikilizaji “waishi mbinguni na duniani kwa wakati mmoja”? Kutofundishwa kwa upana wa maisha ya Kikristo yaliyojaa Roho, yanayofuata Neno, yaliyo na mwelekeo wa maombi, na yenye kujenga wanafunzi? Jaribu kufikiri madhabahu “pasipo maono”.

Mchungaji: Una mashaka kiasi gani kuhusu uwezo wa kile unachofanya sasa? Mashaka mazuri ndiyo nyundo yenye kuvunja madirisha yaliyofunikwa na kiwingu cha mambo yanayowavutia wanadamu. Mashaka aina hiyo ni ishara yenye kuleta matumaini. Bila ya ukiri wa kweli kuhusu mashaka kama hayo, na uchunguzi kwa njia ya maombi kuhusu njia mbadala itolewayo na Mungu, madhabahu unayosimama ndani yake itadumu kutokuwa na maono.

Miaka kadhaa iliyopita, mchungaji maarufu wa Kibaptisti alikuwa kwenye maombi ofisini mwake asubuhi moja. Alikuwa amelala kifudifudi akimwomba Mungu upako wa nguvu za Roho Mtakatifu juu ya huduma yake. Alimsihi Mungu tena na tena, “Ee Bwana! Nipe nguvu Zako. Usiache nihubiri na kufanya huduma pasipo nguvu Zako.” Kila mhubiri wa maana amewahi kuomba sala hii kwa uzito sana na mzigo. Anasema, mara ikaonekana kama paa juu yake limefunguka na mkono ukamshukia na kumgusa kwenye bega. Ikawa ni kama sauti ya Mungu imezungumza ndani yake, hivi: “Mwanangu, acha kuomba!” Alipotulia, Sauti ni kama ilimwambia hivi, “Mwanangu! Kwa mipango yako isivyokuwa mikubwa, huhitaji nguvu Zangu!”

Ewe Mkristo – maono yako ni makubwa kama ya Mungu, kwa ajili ya utukufu Wake? Iko wapi mipango, ndoto, maono, mikakati kwa ajili ya kuifikia dunia nzima – vitu ambavyo kwa kweli vinasukuma rasilmali ya miujiza ya Mungu? Uko wapi mkakati unaotaka miujiza endelevu ili kuudumisha? Yako wapi maono ambayo ni makubwa kiasi kwamba rasilmali za kibinadamu (za aina yoyote na kiwango chochote) hazina uwezo wa kuyategemeza? Maono pekee yenye ukubwa wa umilele ambayo yeyote kati yetu anaweza kuyahitaji yanapatikana katika lile Agizo Kuu ambalo tumepewa na Bwana Yesu Kristo. Kama madhabahu yako haisumbuliwi na maneno “kuwafanya kuwa wanafunzi” na “mataifa yote”, Mungu anawezaje kutazamiwa kuunga mkono kutoka mbinguni? Bila kutatizwa na hilo, madhabahu ya kanisa lako ina ubao unaosema hivi: “hakuna maono”.

Halafu, ni hatua ndogo tu kufikia kwenye viti, watu ambao hawana maono ya kiroho ya hayo. Sheria ya maisha ya ndani ya kanisa ni hii: “watu wako kama mchungaji alivyo”. Watu watapokea jinsi mchungaji wao alivyo kiroho. Hebu tuseme katika mfuatano huu, watu waketio kanisani hawana, au wamepoteza maono yao kuhusu utukufu wa kushangaza sana wa Injili. Inakuwaje? Na wamepoteza uzuri wa pekee wa Yesu Kristo. Inakuwaje? Na wamepoteza maono ya ukuu na utukufu wa kazi yetu ya dunia nzima. Inakuwaje? Na wamepoteza maono ya uwezekano wa kuigusa dunia nzima kwa ujumbe wa Injili na uwezo wa Yesu Kristo kama Wakristo wa kwanza walivyofanya. Inakuwaje? Mtu mmoja amesema, na ni kweli kabisa, “Hatua kutoka aliye tayari kujitoa hadi mtunzaji na hatimaye mzikaji ni fupi sana.”

Kwa nini washirika wa makanisa wanasisimka zaidi kuhusu vitu vingine elfu na zaidi, kuliko kuhusu Mungu, mambo ya kiroho, mbinguni, jehanamu, na umilele? Jibu lake: Hakuna maono, kwa hiyo hakuna motisha. Maana, motisha hutokana na maono.

Kujifunza Injili na Kitabu cha Matendo kwa makini sana kutadhihirisha kwamba Kanisa la kawaida la Kikristo linaendeshwa kwa misingi ya desturi na taratibu kuliko kwa misingi ya kuangaziwa [na Roho Mtakatifu]. Mtu mmoja – kwa mzaha tu – alisema hivi: “Ni vizuri makanisa yafanye na kusema kila kitu kwa usahihi mara ya kwanza, kwa sababu yatafanya na kusema kwa njia hiyo hiyo tangu sasa na kuendelea.”

Maono yanapotoweka katika madhabahu na kwa washirika, tuwe na uhakika kabisa kwamba hayatakuwepo maono ya kiroho katika maisha ya kila siku. Itakuwaje ikiwa Wakristo watapoteza kabisa maono ya nafasi yao kama chumvi na nuru (ktk Mathayo 5:14-16) katika dunia inayoharibika na yenye giza? Itakuwaje kama sisi tutapoteza maono juu yetu kwamba ni wawakilishi wa Yesu Kristo (ktk 2Wakor. 5:20), “katikati ya kizazi kiovu kilichopotoka, ambacho kati yake tunang’aa kama taa duniani, tukilishika na kulitangaza Neno la Uzima” (ktk Wafilipi 2:14-16)? Itakuwaje ikiwa tutapoteza maono yetu juu ya daraja yetu kuu kama “mabalozi kwa ajili ya Kristo”, tulioagizwa kusemea jambo la Mfalme wetu katika dunia hii yenye giza na uhasama? Mbona si kitu cha kufikiri na kukisia kabisa. Kutokuwepo na maono ni kitu kinacho-onekana waziwazi katika madhabahu, kwa washirika, na katika maisha ya kila siku – ukitazama tu mambo yanayotokea, kama yanavyotajwa katika maandiko haya.

MATOKEO YAKE, MAZITO

Hebu fikiri juu ya matokeo mazito yanayofuata hali ile ya kusikitisha sana ya “pasipo maono”. Mahali ambapo hakuna maono, watu huangamia.” Neno linalotafsiriwa “kuangamia” ni la Kiebrania, lenye kushangaza sana. Yaani – limejaa maneno, na linatisha. Lina maana kadhaa tofauti. Maana yake ni “kutokuwa na kujizuia, kujiachilia, kuyeyuka, kuvunjika, kusambaratika vipande-vipande, kutembea uchi, kuangamia.” Sasa, tazama matokeo ya kusikitisha sana ya kupotea kwa maono miongoni mwa Wakristo.

Kwanza – maono yanapokuwa hayapo, watu wa jamii, wa jumuiya, wa kanisa, wa nyumbani “huacha kujizuia”. Hayo ni matokeo ya kiadili ya maono kupotea. Kupoteza maono husababisha vurugu kiadili, ambapo “kila mtu hufanya kilicho sawa machoni pake mwenyewe”. Ona kwamba, kunapokuwa hakuna utambuzi wa uhalisi kamili, watu hufanya “yaliyo sawa machoni pao wenyewe”, wala si kile ambacho kinaonekana kuwa makosa kwao. Kumbuka pia kwamba “sawa” na “kosa” siku zote ni maneno tu kwa wale wenye akili za kawaida au za kimwili. “Sawa” na “kosa” ni vitu halisi kwa wale tu ambao wana akili timamu kiroho. “Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu, lakini mwisho wake ni mauti” (ktk Mithali 14:12). Ona kwamba huyo mtu ana uhakika kwamba njia yake ni sawa – kamwe haoti kwamba njia yake ni ya KiShetani na yenye uharibifu. Hapo tena, tofauti ni katika ufunuo, katika maono na mtazamo wa mtu binafsi. Inashangaza sana kuona jinsi ambavyo watu walio vipofu kwa mambo ya kiroho wanavyohalalisha ukweli wa kuelewa kwao!

Kwamba watu kila mahali siku hizi wameacha kujizuia ni kitu kinachokubaliwa na kila mmoja. Kujitawala, fujo na vurugu na kujiamulia mambo mwenyewe ni mambo yanayozidi kuenea. Tofauti kati ya Mwana wa Mungu na wenye dhambi inadhihirishwa hapo. Yesu alisema hivi: “Siku zote mimi hufanya mambo ambayo yanampendeza Baba Yangu” (ktk Yohana 8:29). Lakini, kauli mbiu ya wenye dhambi (au kiini cha dhambi) ni: “Siku zote mimi hufanya mambo yanayonipendeza”. Pengine atatokea msanii wa siku zijazo atakayetengeneza sanamu au kuchora picha itakayomwonyesha mtu wa karne ya ishirini akiwa amejikumbatia mwenyewe kwa upendo sana, akijipiga busu mwenyewe katika kioo. Lakini, bila ya kupoteza uzito wa hali halisi katika maneno ya utani, hebu maneno ya Shetani aliyopewa na John Milton katika kitabu kinachoitwa Paradise Lost yaturekebishe. Shetani alionyesha ukiri usioepukika wa wenye dhambi wenye kufuata ubinafsi wao bila ya mipaka aliposema hivi: “Mimi mwenyewe ndiye jehanamu”.

Miaka kadhaa iliyopita, magazeti yaliandika kisa cha msaidizi wa fundi uchundo wa Uwanja wa Ndege wa Idlewild huko New York, Marekani. Huyu alikuwa na miaka ishirini, naye alimwandikia rafiki yake mmoja barua, aliyekuwa katika Jeshi la Anga la Marekani katika jimbo la Texas. Barua ilieleza jinsi ambavyo kijana huyo alikuwa ameachana na mchumba wake, na jinsi alivyopanga kuchukua ndege mojawapo ya shirika la Pan American. Akaiba ndege aina ya DC-3 yenye injini mbili, akaanza kuiendesha. Ikashindwa kupaa, ikaanguka, naye akafa. Habari gazetini zilimalizika kwa maneno yake kutoka kwenye ile barua, kwamba, “Nitakuwa nikiendesha mimi mwenyewe, kama ambavyo nimekuwa siku zote – peke yangu.” Kisa hiki hurudiwa tena na tena, katika mavazi tofauti, kila siku – na matokeo ni yale yale. Kujisimamia mwenyewe ni kujiharibu mwenyewe. Mtu anayejisimamia mwenyewe siku zote ataanguka na kuungua! Kwa kuwa mawazo ya wanadamu hupingana sana wakati kila mmoja anapochukuwa sheria yake mwenyewe, machafuko duniani yanaendelea kukua na kuongezeka, na hali ya wasiwasi itokanayo nayo. Mahali ambapo hakuna maono ya mara kwa mara miongoni mwa watu, ambapo hakuna neno lililo wazi kutoka kwa Mungu aliye hai, ambapo hakuna Ukristo halisi wenye maana, basi watu hutupilia mbali vizuizi.

Pili – neno hili lenye nguvu sana la Kiebrania pia linamaanisha “kusambaratika”. “Mahali ambapo hakuna maono, watu husambaratika”. Hayo ni matokeo ya kijamii ya kupoteza maono. Dhambi, inayozidi kuongezeka katika jamii yenye utovu wa maono ya kiroho, ina nguvu ya mvutano fulani. Inawafukuza watu watoke kwenye Kiini cha Kweli cha Uzima ambacho ni Mungu Mwenyewe, na kwa njia hiyo kuwatenganisha wao kwa wao. Basi, tunakuwa na dunia iliyotengana, iliyogawanyikana. Jamii huanza “kulegea, kuyeyuka, kuvunjika, kuwa vipande-vipande”. Neno “kugawanyika” linaelezea hali nyingi tofauti zilizomo katika dunia yetu. Tunazo familia zilizogawanyika, mataifa yaliyogawanyika, dunia iliyogawanyika, na watu wenye haiba zilizogawanyika. Siku moja, daktari wa magonjwa ya akili aliingia kwenye kituo cha mafuta akiwa na gari aina ya pikap. Nyuma alikuwa amebeba viti vitatu. Alipoulizwa anakwenda wapi, alijibu, “Ninakwenda kumtembelea mwenda wazimu (ambaye tatizo lake ni kuona kwamba yeye si mmoja, bali wengi)!” Mara nyingi sana watu binafsi wana”sambaratika”. Binti mmoja msomi wa chuo kikuu fulani alimwambia mwenzake wanayekaa chumba kimoja, “Ninajisikia kama Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe, inayotembea”. Mwenzake akamjibu, “Wala hiyo si kitu. Mimi ni Vita Kuu ya Dunia, inayotembea!” Mtu binafsi anaweza kuvumilia tatizo la aina yoyote ile kama ameunganika ndani, lakini atashindwa na shambulio la aina yoyote ile kama ndani yake mwenyewe kuna ubishi na hali ya kutoelewana.

Habari za Yuda katika Agano Jipya zinamalizika kwa maneno haya: “Basi, mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka, matumbo yake yote yakatoka” (Matendo 1:18). Kama mjuavyo, Yuda alijinyonga, na huku kuharibikiwa kimwili pengine kulitokana na kutokufanikiwa katika kujaribu kujinyonga, au kama matokeo ya kuvimba na kuharibika kulikotokana na maiti yake kuning’inia kwenye kamba yake kwa muda mrefu. Tafsiri ya Biblia Fafanuzi inasema hivi, “Alipasuka katikati ya mwili wake”. Pamoja na kwamba maelezo hayo hayavutii, tunapata picha nzuri. Tafsiri nyingine inasema kwamba Yuda “alisambaratika”. Yaani, “aliachana”. Lakini hii ilikuwa ni tokeo la mwisho la kimwili la yale ambayo yalikuwa yametokea kwa miaka mitatu huko nyuma. Alikuwa ameharibu kile kiini pekee – “saruji” ya KiMungu ambayo ingeunganisha na kushikamanisha haiba yake na kuifanya kamilifu na yenye umoja. Kweli,“alisambaratika katikati”. Na Yuda angefaa kabisa kuwa “mtakatifu mwangalizi” wa majira ya siku hizi. Biblia inatuambia (ktk Wakolosai 1:17) kwamba “vitu vyote hushikamana pamoja” katika Yesu Kristo tu. Lakini, watu wanapopoteza “Maono ya Kuvutia Sana ya Yesu Kristo,” basi jamii inakosa nguvu za kuunganisha, za kufanya vitu kuwa umoja, za kushikamanisha vitu vyote.

Katika mchezo uitwao Green Pastures uliotungwa na Marc Conally, malaika Gabrieli anaonekana akipita hapa na pale katika kumbi na maeneo mbalimbali ya mbinguni, huku akizidi kusumbuka kutokana na vurugu na fujo anazo-ona hapa duniani. Mwishowe anamgeukia Mungu na kusema, “Bwana! Bwana! Inaonekana kwamba kila kitu kilichopigiliwa ili kushikamana kinaanza kuachana!”Watu binafsi na taasisi husambaratika wakati Kristo anapokosa kutawala. Hayo ni matokeo ya kijamii ya upotevu wa maono ya kiroho.

Tatu – hili neno katika Kiebrania lina maana nyingine ya “kutokuvaa” au “kutembea uchi”. Sasa – kwa kuwa kila matumizi ya neno hili yamekuwa ya kiroho, bila shaka maana hii ni ya kiroho pia. Tunapata uwanja mpana kiasi gani kwa ajili ya kujifunza Biblia kama tutaona maana hii kuwa inahusu hali ya kiroho ya wanadamu. Tafsiri kwamba “watu hawajavaa nguo” hudhihirisha matokeo binafsi ya kutokuwa na maono. Katika Biblia – tena kwa mtiririko dhahiri kabisa – kuokolewa kwa wenye dhambi, “kuhesabiwa haki” kwao, ni kitu kinachoonekana kwa lugha ya wao “kuvikwa” na ile haki yenye kulinda na kuhifadhi ya Kristo, na kuhukumiwa kwao kunaonekana katika wao kutokuwa na mavazi na walio wazi kwa ajili ya hukumu. Ukweli ni kwamba, katika Biblia nzima, mavazi ni mfano wa dhambi na haki pia. Mavazi machafu mara nyingi hutumika kama picha ya dhambi na kujihesabia haki, na mavazi safi na meupe hutumika kama picha ya ile haki ya Kristo ifunikayo, inayohifadhi. Ukitaka kufuatilia wazo hilo kwa upana zaidi katika Maandiko, mafungu yafuatayo yatakuwa na maana sana kwako: Mwanzo 3:7, 21; Zekaria 3:1-5; Mathayo 22:11-13; Luka 15:22; Warumi 13:11-14; Waefeso 4:22-24; Wakolosai 3:5-14 na Ufunuo 19:7, 8.

Kitu kimojawapo cha kufurahisha sana katika kuwa Mkristo ni kujua kwamba Mungu amenivika Vazi Bora Zaidi la Mbinguni – tena, kwa gharama Yake Mwenyewe! Hili linaonekana katika simulizi maarufu sana la John Bunyan liitwalo, Safari ya Msafiri. Wakati yule msafiri aliyetambua hatia yake anapofika Msalabani pa Yesu na kumwamini, mzigo wa dhambi zake unamwacha na kuanguka, naye anainuka akiwa anasherehekea msamaha na uzima wa milele. Ndipo anapokutana njiani na “Watatu Wenye Kung’aa” ambao ni mfano wa Mungu baba, Mungu Mwana, na Mungu Roho Mtakatifu. Mungu Baba anamwambia msafiri huyo aliyeokoka, “Amani iwe kwako. Dhambi zako zimesamehewa.” Mungu Mwana anamvua zile nguo chafu alizokuwa amevaa, na badala yake, anampa joho jipya, safi, jeupe. Na Mungu Roho Mtakatifu anaweka alama kwenye uso wake (ambayo ni mfano wa muhuri wa Roho Mtakatifu), na kumpa mkononi mwake gombo lililokunjwa vizuri (ambalo ni mfano wa Biblia).

Hiyo kazi ya pili – kazi ya kumvua mwenye dhambi mavazi yake ya kale na kumvika upya – ndiyo inayolengwa wakati andiko letu la msingi linaposema, “Mahali ambapo hakuna maono, watu hawana mavazi.” Tunasoma hivi katika Yohana 3:36, “Yeye amwaminiye Mwana anao uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali hasira ya Mungu inakaa juu yake.” Mwamini anayemtumaini Kristo amefunikwa kwa haki ya Kristo naye huepuka hasira ya Mungu kuhusu dhambi. Lakini, mwenye dhambi asiyeamini hana nguo, na kwa hali hiyo, yuko wazi kupatikana na kila kitu kinachotaka kumharibu.

“Mahali ambapo hakuna maono,” watu zaidi na zaidi hubaki “bila nguo” au, pasipo ulinzi kwa kitambo na milele. Hayo ndiyo matokeo binafsi ya kutokuwa na maono.

Mwisho, neno la Kiebrania linatafsiriwa kwa usahihi kabisa hapa. Maana yake ni “kuangamia”. “Mahali ambapo hakuna maono, watu huangamia.” Kweli, huruma inahitajika hapa kwa sababu, kilicho hatarini ni “watu”. Wangekuwa wanyama au mimea, mambo yasingekuwa mabaya sana. Lakini ni watu – kama wewe na kama mimi. “Wanaangamia”. Katika Yohana 3:16, neno “kuangamia” linawekwa kinyume na kuwa na “uzima wa milele”. Kuangamia maana yake ni kuhusika milele katika kifo hai na maisha ya kufa katika mahali paitwapo jehanamu. Hapo hapo tena, 1Wakor. 1:18 inaonyesha kwamba watu wasiokuwa na Kristo wako katika hali ya sasa ya kuangamia. Huku kuangamia kwa watu ni matokeo ya kiroho na ya milele ya kutokuwa na maono katika Wakristo. Watu watatu huangamia pasipo Kristo kila sekunde, na Kanisa kwa sehemu kubwa limepoteza maono yake! Jehanamu inajaa, na Mbingu bado ina nafasi tele za kujazwa! Yote kwa sababu maono ya Kanisa yamechuja!

Zamani kidogo, mfanya biashara tajiri alisafiri kwenda India kuwinda simba marara wa Bengali. Akakaa huko majuma sita. Aliporudi nyumbani, alihudhuria ibada ya katikati ya juma katika kanisa lake kubwa sana. Alikuta wanajadili kuhusu bajeti ya mwaka ya kanisa. Mfanya biashara huyo alishtua kanisa zima kwa kutoa pendekezo kwamba sadaka zote kwa ajili ya utume wa nchi za nje ziondolewe kwenye bajeti. Mzee mmoja akauliza sababu ya pendekezo hilo la ajabu sana. Jibu likatoka, hivi: “Ndiyo nimerudi kutoka safari ya majuma sita huko India, na katika kipindi chote hicho, sikuona mishenari hata mmoja.” Yule mzee akauliza tena, “Na kusudi la safari yako hasa lilikuwa nini?” Jibu: “Nilikwenda kuwinda simba marara wa Bengali.” Akaulizwa, “Na ulifanikiwa kuona wangapi?” Akajibu, “Niliwaona sita.” Yule mzee akasema, “Hiyo ni ajabu kabisa. Mimi nimekaa India miaka kumi na tatu kama mishenari, na niliwaona wamishenari mamia kwa mamia. Lakini mpaka sasa sijaweza kumwona simba marara mmoja wa Bengali huko India!” Kwa hiyo, mengi sana yanategemeana na mtazamo wetu, na maono yetu.

Maneno ya Mithali 29:18 yaliandikwa na Mfalme Sulemani, mtu ambaye katika utawala wake, maono yalipotea. Na hapakuwa na kushindwa kubaya zaidi katika historia ya Israeli kuliko kule kwa Sulemani. Watu walisambaratika! Taifa liliporomoka! Ufalme uligawanyika!

Basi, uchaguzi mbele yetu ni dhahiri kabisa: Aidha ni “maono au mgawanyiko”! Hii ni kweli duniani kote, kitaifa, katika mahali pamoja, lakini sana ni kweli katika Kanisa la Yesu Kristo na katika maisha ya Mkristo binafsi!

Ni lazima – na ni lazima – tumngoje Mungu katika utulivu na maombi, tukiwa na hali ya ndani sana ya uhitaji na moyo wenye kufundishika, na kumwomba Yeye arejeshe maono ya Utukufu Wake mkuu sana, naya Mpango Wake mkuu mno kwa ajili yetu, na dunia! Maono yanaporejezwa, tutagundua tena kwamba Mpango Wake wote umefunuliwa katika Agizo Kuu la Bwana wetu, na kwamba jukumu hapo ni “kuwageuza watu wawe wanafunzi”.

Dawson Trotman alikuwa sawa aliposema hivi: “Maono ya kiroho ni kupata moyoni mwako kile kilicho kwenye moyo wa Mungu – yaani, dunia!” Paulo aliomba kwamba Wakristo wa Kolosai wapate “kuona mambo kwa mtazamo wa Mungu” (ktk Wakolosai 1:9, TLR). Kama tungefanikiwa hapo, yangekuwepo mapinduzi makubwa sana!

“Mtu mmoja aliyeamka

Anaweza kumwamsha mwingine;

Na huyo wa pili anaweza kumwamsha

Ndugu yake aliyeko jirani.

Hao watatu walioamka

Wanaweza kuamsha mji mzima

Kwa kugeuza hapo pote

Juu chini.

Wengi walioamka

Wanaweza kufanya vurugu

Kiasi kwamba hatimaye

Sisi wote tunaamshwa.

Mtu mmoja aliyeamka,

Alfajiri ikiwa machoni mwake,

HUONGEZEKA!”

Sura Ya 2

Agizo Lenye Kuamua Wajibu Wetu

“Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.”

Mathayo 28:18-20

Tunapoondoka nyumbani, mara nyingi tunatoa maagizo yetu muhimu sana na maelezo – mambo ambayo hatutaki watu wengine wasahau. Mke wangu mimi huyaweka mezani au kwenye mlango wa friji. Nini maana yake? Kwamba, hayo ni muhimu!

George Peters katika kitabu chake kiitwacho A Biblical Theology of Missions aliandika hivi: “Agizo Kuu ndiyo taa yenye kutuongoza katikati ya ukungu wa kibinadamu na mawazo. Tunahitaji sana kujifunza upya na kwa undani sana Agizo Kuu. Ni waalimu wachache sana na wafafanuzi wanaoshughulika kwa upana sana na mafungu yanayohusu Agizo Kuu. Kanisa linahitaji kufikiri upya na kwa uzito sana lile Agizo la kufanya watu kuwa wanafunzi.” Mishenari mstaafu John McGee aliyefanya kazi huko Nigeria, alisema hivi: “Kuna mengi sana katika Agizo Kuu kuliko mtu anavyoweza kuota, au kufikiri, au kutenda, hata kama angekuwa na uwezo wa kuishi mara kumi.”

Katika fungu la Maandiko ambayo ni pamoja na Agizo Kuu (ktk Mathayo 28:16-20), tunasoma kwamba “wale wanafunzi kumi na moja wakaenda Galilaya hadi kwenye mlima ambao Yesu alikuwa amewaagizia.” Huku ndiko kuonekana kwa Yesu kwa kipekee baada ya ufufuo ambako kulikuwa kumepangwa kabla. Alipoonekana mara zile nyingine zote, alikuwa anatokea tu. Bila shaka kulikuwa na kitu fulani cha muhimu sana alichotaka kukisema au kukifanya wakati huu. Na kweli, ndivyo ilivyokuwa! Hapa “alibandika” maagizo Yake ya Mwisho. Kuna msemo mmoja wa kawaida sana miongoni mwa watu wenye kutumia vyombo aina mbalimbali – “Kila Kitu Kikishindikana, Soma Maelekezo”. Katika sura hii, tunakwenda kujifunza na kusoma Maelekezo Yake ya Mwisho. Tutagawanya maelekezo hayo katika mafungu mawili: Uhakikisho Ulioko Katika Hilo Agizo, na Kazi Iliyoko Katika Hilo Agizo. Ikiwa tunataka kuelewa na kutimiza Agizo Kuu, ni lazima tuchunguze kwa makini sana mambo hayo mawili.

UHAKIKISHO ULIOKO KATIKA HILO AGIZO (MS. 18, 20A)

Agizo lenyewe linaanza kwa tamko la kushangaza sana lililowahi kutolewa. Yesu alisema, “Mamlaka yote nimepewa Mimi,mbinguni na duniani.” Hapo, sifa Yake na agizo letu vinategemea sentensi hiyo. Nini maana yake, na ni muhimu kiasi gani maneno hayo?

“Mamlaka” yanayotajwa hapa ni mamlaka ya KiMungu. Kanuni kuu katika Maandiko yote ni kwamba, “hakuna mamlaka isipokuwa itokayo kwa Mungu” (ktk Warumi 13:1), na kanuni hiyo inaonekana hapa pia. Katika Kiyunani, neno linalotumiwa kueleza mamlaka ni exousia, ambalo maana yake halisi ni “kutokana na kuwa”. Fikiri kidogo jambo hili. Maana yake ni kwamba mamlaka yote ya lazima kutoka kwa Mungu mwenyewe yametolewa kwetu kwa njia ya mahusiano yetu na Kristo ili kutimiza Agizo hilo.

Halafu, mamlaka hii ni mamlaka iliyotolewa. Yesu Kristo anayo mamlaka katika Nafsi Yake, ambayo anaimiliki kwa sababu ya kuwa Yeye. Mamlaka aliyokuwa nayo wakati wa maisha Yake hapa duniani ilionyeshwa kwa njia nyingi zilizo wazi.

Alionyesha mamlaka Yake juu ya nguvu za asili wakati alipotuliza dhoruba kali iliyokuwa imewatisha hata wavuvi waliozoea, kwa neno tu la kinywa Chake na kunyoosha mkono Wake. Alikuwa amesema na mtini nao ukakauka mbele ya macho ya wanafunzi, waliokuwa wameshangaa sana.

Vile vile alikuwa na mamlaka juu ya dhamiri ya mwanadamu. Kwa kutumia mazungumzo rahisi tu naye, Mwokozi wetu aliamsha dhamiri ya mwanamke Msamaria aliyekuwa amejaa dhambi, na kuanzisha hali ya matumaini katika nafsi yake. Wakati mwingine, akiwa amezungukwa kabisa na kundi lililotaka kujua mambo mengi, kwa kutaja tu jina la mtu na kumwambia ashuke kutoka kwenye mti, aliweza kuiamsha dhamiri ya Zakayo, Myahudi aliyechukiwa na asiyemcha Mungu, wa mjini Yeriko.

Vile vile alionyesha mamlaka makuu juu ya ile dunia ya kiroho isiyoonekana wakati wa maisha Yake hapa duniani. Kwa neno tu au mguso, aliweza kufukuza falme na mamlaka za uovu zilizokuwa zimetawala maisha ya mtu.

Tena alikuwa na mamlaka ya kupendeza sana katika eneo la udhaifu na magonjwa ya mwanadamu. Akitumia nguvu Zake bila kutaka kujionyesha, lakini kwa ajili ya kusaidia maisha ya watu waliokuwa wanateseka, aliwafanya viziwi wasikie, vipofu waone, bubu waseme, viwete watembee, vilema wanyooke katika viungo vyao, na wafu warudie uhai wao.

Hata mafundisho Yake pia yalikuwa na mamlaka. Baada ya mafundisho Yake ya kwanza katika sinagogi fulani, watu “walishangazwa na mafundisho Yake, kwa sababu aliwafundisha kama mtu aliyekuwa na mamlaka, si kama waandishi” (ktk Marko 1:22, TLR). Yesu hakusita kuchukua mamlaka kamili kabisa. Alidai kuwa na mamlaka ya kusamehe dhambi (ktk Marko 2:10). Alitoa matamko yaliyorekebisha kanuni za Torati ya Musa, ambayo kila mtu aliikubali kuwa ilitokana na Mungu (ktk Mathayo 5:21, 27, 33). Hata alidai kwamba Yeye Mwenyewe ndiye angemhukumu kila mtu (ktk Yohana 5:27).

Lakini, mamlaka inayoonekana katika madai haya si ile mamlaka inayotajwa katika Mathayo 28:18. Yesu alisema kwamba haya mamlaka “yametolewa” bila shaka kwa msingi wa mafanikio Yake katika Kifo na Kufufuka Kwake. Mamlaka ambayo alikuwa nayo wakati huo katika utukufu Wake wa ufufuo yalizidi sana yale aliyokuwa nayo wakati wa maisha Yake. Kila aina ya mamlaka ilikuwa Yake kwa sasa. Mamlaka hiyo alikuwa amepewa kwa amri ya Baba Yake mbinguni. Wanafunzi walijua kwamba wao walikuwa watumishi wa Bwana ambaye mamlaka Yake mbinguni na duniani haikuwa na utata hata kidogo wala swali la aina yoyote ile. Tunasoma hivi katika Warumi 1:4, “Alitangazwa kuwa Mwana wa Mungu kwa nguvu (mamlaka) … kwa ufufuo kutoka kwa wafu” (TLR). Hayo mamlaka ndiyo msingi wa Agizo analotoa kwa wanafunzi Wake.

Ni dai la ajabu sana! A.T. Robertson alisema hivi: “Ni onyesho la hali ya juu sana katika historia ya dunia, kumwona Kristo aliyefufuka, pasipo fedha wala jeshi wala taifa, akiwaagiza kundi hili la watu mia tano – waume kwa wake – waende kuiteka dunia na kuwafikisha mahali pa kuamini kwamba inawezekana kufanyika, kwa mguso na udhati na nguvu.”

Vile vile, mamlaka hii ni mamlaka anayostahili Yeye. Yesu alisema hivi: “Mimi nimepewa mamlaka yote.” Ona kwamba hii mamlaka hatujapewa sisi, bali kapewa Yeye. Lakini, hilo lisitupe hofu, kwa sababu chochote kilicho Chake ni mali ya kila mtu aliyeokoka. Kila mtu aliyezaliwa mara ya pili ni mrithi wa Mungu kwa sababu yeye ni “mrithi pamoja na Kristo” (ktk Warumi 8:17). Kila kitu katika milki ya Baba ambacho kihalali ni mali ya Kristo kwa sasa ni mali yangu pia kwa sababu ya mahusiano yangu kiimani, au kujitambulisha kwangu kiimani, na Yeye. Chochote kilicho Chake ni changu, si kwa sababu mimi ninastahili kuwa nacho, bali kwa sababu mimi niko ndani Yake. Ona pia kwamba, hakupewa mamlaka haya kwa sababu Yeye ni Mwana wa Mungu. Kama Mungu, hakuna kitu anachoweza kuongezewa, na hakuna kitu kinachoweza kupunguzwa Kwake. Mamlaka ambayo Yesu anadai hapa ni mamlaka ambayo ameipata (ameistahili) kama Mwana wa Mtu. Neno “aliyopewa” linaonyesha tendo la wakati uliopita, na bila shaka humaanisha kukabidhiwa mamlaka hiyo siku ile alipofufuka toka kwa wafu. Hii inakubaliana na yale maandiko katika Wafilipi 2:5-11, yanayohusu Kunyenyekezwa na Kutukuzwa Kwake. Baada ya Paulo kuonyesha jinsi Yesu alivyoshushwa na kunyenyekezwa, ndipo anapodhihirisha kutukuzwa Kwake kulikofuata. “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” (ktk Wafilipi 2:9-11). Kwa hiyo, kutukuzwa Kwake na mamlaka Yake vilimstahili kutokana na kifo na kufufuka Kwake.

Mwisho – mamlaka aliyodai kabla ya kutoa Agizo Lake Kuu yalikuwa mamlaka yaliyoelezwa na kuwekwa wazi. “Nimepewa mamlaka yote, mbinguni na duniani.” Maeneo hayo mawili yanayotajwa ndiyo pekee ambayo sisi tunahusika nayo, na bila shaka Yesu Kristo anatenda kazi katika maeneo hayo pia. “Mbinguni na duniani.” Mamlaka yote ya mbinguni ni Yake, na mamlaka yote ya duniani ni Yake. Anawatangazia wanafunzi Wake kwamba “nimepewa Mimi mamlaka yote mbinguni”, mahali alipopokea “Jina lipitalo majina yote”, mahali ambapo “ametukuzwa na kuketishwa mkono wa kuume wa mamlaka”, mahali ambapo “ametiwa taji ya heshima na utukufu”. Anatangaza pia kwamba “Mimi nimepewa mamlaka yote duniani”. Hivyo, Yeye ndiye Bwana mkuu wa kote kuwili.

Katika mchezo maarufu sana wa Shakespeare, mwandishi Mwingereza maarufu, anaonekana Liwali wa Kent akimjia mfalme kwa siri, akiwa amejibadilisha. Mfalme huyo Lear anamwambia, “Unataka nini wewe?” Yule Liwali anamjibu, “Nataka nikutumikie.” Mfalme anamwuliza, “Kwa nini?” Ndipo linatoka jibu maarufu la Liwali wa Kent, kwamba, “Kwa sababu katika uso wako naona kitu ambacho kwa hiari yangu mwenyewe naweza kukiita bwana”. Mfalme akamwuliza, “Kitu gani hicho?” Liwali anajibu, “Mamlaka”.

Yesu anatoa madai halali kabisa kwamba mamlaka yote ni Yake. Na katika mamlaka hiyo ndipo tunapaswa kutekeleza ule mradi wa utume (na ile amri ya kufanya watu kuwa wanafunzi). Mamlaka Yake hayajapungua wala kumalizika kutokana na miaka kupita. Basi, kwa msingi wa mamlaka hiyo, tunapaswa kutekeleza agizo au kazi tuliyopewa katika Agizo Kuu.

KAZI ILIYOKO KATIKA HILO AGIZO (MS. 19, 20)

AMRI PEKEE KWA KANISA (KWA MKRISTO) KUSONGA MBELE

Agizo Kuu ndiyo “amri pekee ya kusonga mbele” iliyowahi kutolewa na Yesu Kristo kwa Kanisa Lake. Agizo Kuu ni kazi ya kuvuna roho na utume, lakini ni zaidi ya hayo. Kuna maelezo kuhusu Agizo Kuu la Bwana wetu katika Agano Jipya mara tano. Linatajwa kwa njia tofauti katika Mathayo 28:18-20 (kwa maelezo yaliyo dhahiri zaidi), katika Marko 16:15 (kwa kifupi lakini wazi), katika Luka 24:47, Yohana 20:21 na Matendo 1:8 (kwa ufafanuzi mpana zaidi).

Katika maelezo ya Mathayo, Kanisa la Yesu Kristo linapata msingi kwa ajili ya kazi yake. Hakuna swali kabisa katika maneno anayotoa Mathayo kuhusu kile ambacho Yesu alikusudia wafuasi Wake kufanya. Si swala la hisia au kujisikia. Si kazi ya kufanywa tutakapoona inafaa. Yesu aliacha maagizo dhahiri. Maagizo hayo ni kamilifu (yaani, hayapitwi na wakati wala kubadilika) na ni ya mara moja. Agizo Kuu ni la sasa hivi, na linamfunga kila Mkristo kulitimiza wakati huu. Maneno ya Agizo hili ni maneno tendaji: Enendeni, fanyeni watu kuwa wanafunzi, batizeni, na fundisheni. Kwa kifupi tu, Kanisa liko chini ya amri, lakini uhalisi wa hiyo amri unaweza kuwashangaza waamini wengi.

KULIGAWA AGIZO SEHEMU SEHEMU

Ningependa kuligawa Agizo Kuu katika sehemu saba. Muhtasari ni kama ifuatavyo: Kwanza, sisi tunawajibika kutumia kila mtenda kazi anayepatikana (neno “ninyi” la ms. 19 liko katika wingi). Halafu, tunatakiwa kuingia shambani (“enendeni”). Tatu, tunatakiwa kila wakati kupanua maono yetu (“mataifa yote”). Nne, tunapaswa kuwashuhudia wahusika (“kufanya wanafunzi”). Tano, tunapaswa kuwahusisha walioshuhudiwa (“mkiwabatiza katika jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu”). Sita, tunatakiwa kuwaelimisha na kuwajenga waliojiunga nasi (“na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi”). Na mwisho, tunapaswa kutarajia Yeye kutenda kazi (“na tazama, Mimi niko pamoja nanyi siku zote, hata mwisho wa dunia”). Bila shaka unaona sasa kwamba, yapo mengine mengi sana kuhusu Agizo Kuu la Bwana wetu kuliko ambavyo sisi tumekuwa tukiheshimu!

Tunapochunguza kwa makini na dhati kabisa hili Agizo, tunagundua kitu cha kushangaza sana. Tunapata kwamba, kwa karibu karne mbili, Agizo lilifanya kazi vizuri kabisa na kuigusa dunia iliyokuwa inajulikana siku zile kwa haraka sana. Lakini, kitu cha ajabu kikatokea. Kitu fulani kiliharibika kabisa. Ili kuona hilo, ningependa tutazame kila hoja katika zile saba ambazo nimetaja. Chini ya kila hoja, ninataka utazame vichwa vidogo viwili. Kimoja ni “Mkakati wa Mwokozi”, na kingine kinaitwa “Mbadala wa Shetani”. Tutafanya hivyo na kila hoja.

1. KUTUMIA KILA MTENDA KAZI

Hoja ya kwanza katika Agizo Kuu ni kutumia kila mtenda kazi. Katika mstari wa 19, neno “ninyi” liko katika wingi, na maana yake hasa ni “ninyi wote”.

Mkakati Wa Mwokozi

Mtu mmoja ameeleza nia ya Yesu kuhusu kutimizwa kwa Agizo hili Kuu kwa maneno haya: “Waamini wote wanatakiwa kuhusika, na wanapaswa kutenda wakati wote”. Kitu kimoja – licha ya nguvu za Mungu – kilichofanya Agizo Kuu kufanikiwa sana hapo mwanzoni ni kwamba, watenda kazi wake wote walihusishwa kufanya huduma mahali palipotakiwa. Lengo lilikuwa kwamba kila mwanafunzi awe mzalishaji wa wavuna roho na wafanya watu kuwa wanafunzi kama yeye. Wote walikuwa wasemaji, waenezaji na wainjilisti! Ukweli ni kwamba, kushiriki kulikuwa kwa kila mtu miongoni mwao mpaka ikabidi sheria ziwekwe ili kuondoa vurugu au kuchanganyikiwa (ona 1Wakor. 14:31). Hapakuwepo na watazamaji miongoni mwao. Adolph Harnack, mwanahistoria maarufu wa kanisa, alisema hivi: “Wakati kanisa liliposhinda sana katika siku za mwanzo za Dola ya Rumi, halikufanya hivyo kwa waalimu au wahubiri au mitume, bali kwa wamishenari wa kawaida kabisa.” Hili Agizo linataka huduma binafsi kutoka kwa kila aaminiye. Wote walio viungo vya Mwili wa Kristo hawawezi kufanya hivyo bila ya kila mshirika kufanya hivyo. Kanisa moja katika eneo la Manhattan huko Marekani lina ujumbe ufuatao kwenye kibao chake: “Mchungaji, --------“. “Wahudumu: Kila mshirika.” Huo ndiyo mkakati wa Mwokozi kwa ajili ya kila mtenda kazi kutumika.

Mbadala Wa Shetani

Sasa, tazama mbadala alioleta Shetani. Ukweli ni kwamba Agizo Kuu lilifanya kazi. Yaani, lilifanya kazi mpaka Shetani akaona vibaya. Lilifanya kazi vizuri sana kiasi kwamba ilimchukua miaka 200 kuondokana na kipigo alichopata na kupanga upya majeshi yake. Hatimaye, akapambana na Agizo Kuu kwa mpango mbadala wake. Si vigumu kuona kwamba Agizo Kuu la kwanza limevurugwa kiasi. Limerekebishwa, na kwa karne nyingi sana, makanisa mengi yameangukia katika mpango wa Shetani. Pigo kubwa sana la Shetani dhidi ya Agizo Kuu lilielekezwa kwenye ile hoja ya kwanza, ya kutumika kila mtenda kazi.

Mapema kabisa katika historia ya Kanisa, Shetani alianzisha mgawanyo katika Kanisa. Likawa na sehemu mbili, naye akakazia kupita kiasi zile tofauti. Walio wengi aliwaita “walei – wasiokuwa wachungaji” na wale wachache akawaita “wachungaji – watumishi”. Na hoja yake kubwa ilikuwa kwamba walei hawana uwezo na hawana vipawa, na kwamba hawahusiki katika kazi halisi ya kanisa hata hivyo. Shetani basi akasimamia ujenzi wa tabaka ya watu wa dini walio wataalamu. Hawa wataalamu walitakiwa (1) kupigana vita zote za kiroho, na (2) kufanya kazi zote za kiroho. Vipi shughuli ya “walei”? Kumtegemeza na kumsaidia huyo mtaalamu kiongozi na kulipia mpango wake kufanyika (ambapo katika Agano Jipya, watu ndiyo mpango mkuu).

Basi, “ngazi ya kiroho” ikatengenezwa Kanisani. Juu kabisa ya ngazi alikuwepo “mishenari”, halafu anayefuata ni mchungaji, halafu watendaji wengine wataalamu wa kidini, na mwisho wa ngazi, mshirika wa kawaida. Kuna mtu amesema kwamba kizazi chetu ni “kizazi cha mtazamaji”. Mpira wa miguu una wachezaji 22 kwa mara moja, lakini unaweza kuwa na watazamaji mamilioni wakati huo huo! Michezo mingine ina wachezaji 18. Mpira wa vikapu una wachezaji kumi, ngumi wachezaji ni wawili, na kuna michezo mingine katika Olimpiki yenye mchezaji mmoja tu. Lakini michezo hiyo yote ina mashabiki mamilioni. Mchekeshaji mmoja aitwaye Fred Allen alisema hivi: “Kama jamii itaendelea kama ilivyo, baada ya muda tutakuwa na dunia iliyojaa watu wenye macho makubwa kama sahani za vikombe vya chai, na akili zenye ukubwa wa harage” (kwa kuwa wakati wote watu wanakodoa macho, na kutumia muda mwingi katika ushabiki)!

Matatizo Kanisani Ya Watu Kutokuwa Na Kazi, Na Kazi Kidogo

Kanisa limetengeneza matatizo mawili ya “kutokuwa na ajira” na hayo yanaungana mkono mara zote, na kufanya mambo kuwa mabaya zaidi. Kuna tatizo la kutokuwa na kazi kwa washirika katika kusanyiko la mahali. Kwa kuwa mshirika wa kawaida katika kanisa la kawaida hatimizi kazi yake aliyopangiwa na Mungu, “mshahara” wake unapunguzwa na kuwa posho tu kwa ajili ya kuishi. Wajibu wake hautimizwi, thawabu yake inapotea, dunia inabakia gizani, na Shetani anatosheka vizuri sana.

Halafu kuna tatizo linalokaribiana na lile, ambalo ni mtumishi kutofanya kazi ipasavyo. Mchungaji wa kawaida katika kanisa la siku hizi ana kazi nyingi, lakini hafanyi kazi ipasavyo! Wakati Henry M. Stanley aliporudi kutoka Afrika kwenye kumtafuta David Livingstone, mwanahabari mmoja alimwuliza swali hivi: “Ni kitu gani kilichokusumbua zaidi wakati ukiwa Afrika? Ni wale simba, au ni nyoka?” Stanley akajibu hivi, “Wala! Walionisumbua zaidi ni mbu!” Wachungaji wetu hawapati kuona simba na chui kwa sababu daima wako kwenye mapambano na mbu. Wakati vita kuu za atomiki zinapiganwa katika ulimwengu wa roho, wao wanajitahidi kupambana na kukabiliana na mashambulizi ya mbegu ndogo ndogo tu! Ongezeko la vitu vingi vidogo vidogo – vishughuli vingi vya kidini ambavyo vinachokesha, pamoja na picha bandia ya huduma ya mchungaji ambazo zimechorwa njiani mwake vinamfanya mchungaji ashindwe kutekeleza kazi pekee ambayo Mungu amempa.

Hivi karibuni nilipata taarifa kutoka Ofisi Kuu ya Jimbo kwamba wachungaji 300 wa Kibaptisti wanaondolewa makanisani kila mwezi. Sina uhakika na idadi hiyo, lakini najua kwamba tatizo hilo ni kubwa sana. Pia nilisikia taarifa miaka kadhaa iliyopita kwamba wachungaji zaidi ya elfu moja wa Kibaptisti wanaachana na madhabahu zao. Sina uwezo wa kuthibitisha idadi hiyo, lakini najua kwamba tatizo hilo ni kubwa sana pia. Pengine sababu kubwa ya huko kutatizika kwa uongozi unaoitwa ni kwamba kiongozi huyo hatosheki kwa “ajira ndogo” inayomkabili – hana kazi za kumtosha kuridhika!

Ukristo Tazamaji Katika Kanisa

Tumetengeneza Ukristo tazamaji katika kanisa, ambao katika huo, wachache ndiyo wasemaji, na wengi ni wasikilizaji. Kanisa limejaa “umoja wa mashabiki” – mashabiki wa imani. Hebu fikiri kuhusu duka la kuuza vitu jumla, ambalo lina meneja mauzo ambaye kazi yake ni kuuza hivyo vitu na kufundisha kuhusu sifa ya vitu hivyo na mbinu za uuzaji. Tuseme pia kwamba duka hilo lina kundi kubwa tu la “wauzaji” ambao kazi yao kubwa ni kuwatafuta wasikilizaji na kuwatia moyo kusikiliza tu mafundisho ya meneja mauzo. Kingekuwa kituko cha namna gani hicho? Je, duka hilo lingedumu kwa muda gani? Ndugu James S. Stewart wa Edinburgh, Uskochi, alisema hivi: “Tatizo hasa la Ukristo si wasemao hakuna Mungu wala wenye mashaka, bali ni Mkristo asiyeshuhudia, asiyezaa matunda, anayejaribu kuingiza roho yake mbinguni kwa njia ya magendo, yeye mwenyewe.” Huo ndiyo mkakati wa Shetani, na zaidi ya hayo, ametumia sana neno “ninyi” mpaka imefikia kwamba hata hao “watumishi” si wote wanaoshuhudia!

Hebu tazama jamii ya Kikristo. Kanisa liko upande gani – upande wa Mkakati wa Mwokozi, au upande wa Mbadala wa Shetani? Nadhani jibu liko wazi kabisa, na linasikitisha. Ni lazima tutazame upya Amri yetu ya Kusonga Mbele!

2. KUINGIA SHAMBANI

Hoja ya pili katika muhtasari wetu kuhusu Agizo Kuu ni kuingia shambani kote. Neno “enendeni” ni neno tendaji, lenye nguvu – neno linalo-onyesha kwenda au kutembea.

Mkakati Wa Mwokozi

Mkakati wa Mwokozi ni dhahiri. Katika Mathayo 13:38, alisema hivi: “Shamba ni dunia”. Hili si shamba kwa ajili ya kanisa, bali ni shamba kwa ajili ya kanisa lako la mahali! Yesu Kristo anakutazamia uhusike na dunia nzima! Mifano ambayo Yesu anatumia kusema kuhusu Wakristo na Injili imefungamanishwa pamoja kwa kitu kimoja. Yote ina tabia ya kupenya – kuingia ndani. Yesu alitumia mfano kama nuru, chumvi, funguo, mkate, na maji. Nuru haina faida kama haipenyi na kufukuza giza. Chumvi haina faida kama inabakia ndani ya chupa yake. Lazima ipenye na kuingia katika mboga au viazi. Mtoto mmoja mvulana alisema hivi, “Chumvi ndiyo huharibu viazi – ukiacha kuiweka.” Funguo hazina maana kama haziingii katika kitasa. Mkate hauna faida ukiwa nje ya mlaji, na maji hayatoshelezi hitaji la mtu mwenye kiu kama yasipomwingia. Vivyo hivyo, Wakristo wanatakiwa kuingia na kupenya duniani kila mara.

“Huwezi kumtaja Mungu bila kwenda. Hakuna uzuri bila kwenda. Huwezi kutamka neno Injili bila kwenda, na huwezi kuitii Injili na kuwa mtumishi mzuri wa Mungu usipokwenda – kwa masharti Yake. Ukristo ni kitu cha kwenda kwa asili yake na msukumo – si cha kushikilia. Kila Mkristo anapaswa kuishi kikazi (yaani, kama Mkristo) kwenye eneo la kupenya – iwe ni katika maabara ya kisayansi, maktaba, kiwandani, shamba la matunda, kazi ya kugawa vitu, cheo kikubwa, kwenye ndege ya kisasa, katika hospitali ya tabibu wa magonjwa ya akili, au katika ofisi ya mchungaji. “Dunia” yetu ni popote tulipo, penye watu. Katika Luka 10:1-3, Biblia inatuambia, “Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, ‘Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni. Angalieni, nawatuma kama wanakondoo kati ya mbwamwitu”. Ona maeneo ambayo nimekazia kwa kutumia wino mwepesi. Maneno hayo yamejaa! Kila Mkristo anapaswa kuwa mwanzilishi, mtangulizi kwa ajili ya ujio wa Kristo “kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe.” Wanakondoo kati ya mbwamwitu watarajie kupona kwa muujiza tu!

Tena – neno “enendeni” katika Agizo Kuu SI AMRI. Kulihesabu kwamba ni amri ni kuendeleza ile dhana ya “ngazi ya kiroho katika Ukristo”. Lingekuwa ni amri, kila ambaye angekwenda mbali ili kuihubiri Injili au kumshuhudia Kristo angehesabiwa kuwa mtu maalum. Lakini, neno tendaji lina maana hii: “Mnapokuwa mkienda”, au hata, “Kwa kuwa mnakwenda”. Yesu asingekosa akili kiasi hicho, atuagize kufanya kitu ambacho tunafanya tayari! Je, kanisa lako liko wapi Jumanne mchana saa tisa? Kwani liko kanisani? Hapana, “linakwenda”. Swala hapa si kwamba mbona kanisa haliendi duniani? Swala ni hili: Je, kanisa linatimiza kazi yake linapoingia na kupenyeza?

Nilikuwa katika mji mkubwa mzuri sana katika nchi ya kigeni fulani, miaka kadhaa iliyopita. Nilihubiri kwenye kanisa la Kiingereza hapo Jumapili asubuhi. Nikawahi ili nipate nafasi ya kuzungumza na watu walipokuwa wanafika ibadani. Mbona nilishtushwa sana na watu wenyewe! Walikuwepo Wamarekani wengi, na walikuwa wafanya kazi katika shirika la mafuta la kimataifa, wenye mishahara mikubwa sana. Nilipowauliza jinsi walivyokuwa wanafurahia kukaa huko, wote walilalamika kwamba wanachoshwa na mambo yale yale kila siku. Wengi wao walikuwa hapo kwa mikataba ya miaka miwili. Katika mahubiri yangu, niliuliza ni kwa nini wasijifunze lugha ya pale na wawe na vipeperushi vyenye ujumbe wa Injili katika lugha ya pale na wafanye umisheni, uinjilisti na kuleta watu kwa Yesu wakiwa huko. Nadhani walipuuza wazo hilo bila hata ya kulifikiria! Ni hivi: Kuna mtu ambaye ametuuzia wazo baya kabisa lenye kupelekea usaliti mkubwa sana wa Yesu na Agizo Lake. Wao walikuwa “wamekwenda” (tena, kwa kulipwa na shirika la mafuta), lakini hawakutambua wajibu wao “wakiwa katika kwenda”.

Mbadala Wa Shetani

Shetani ameingiza mbadala wa kijanja na siri sana katika akili za Kanisa. Maneno makuu mawili katika Injili ni “njoo” na “enenda”. Tukisha kuja kwa Kristo (Mathayo 11:28-30, kwa mfano), tunapaswa “kwenda na kuwaeleza” watu wote yale tuliyopata katika Kristo. Shetani ni bingwa wa kutumia watu, na kubadili maneno. Yeye akaingiza upotofu wa polepole kanisani, kuliondoa kwenye “nenda ukaeleze” na kulitia kwenye “njoo usikie”. Mkomunisti mmoja alitania Kanisa kwa maneno haya, “Kauli mbiu ya Wakristo inaonekana ni, ‘Njooni hapa mpate ujumbe wa Mungu, mwende mbinguni. Au acheni kuja, mwende jehanamu’!” Ndugu mmoja aitwaye Paul Little alisema hivi, “Tatizo si kwamba Injili imepoteza nguvu yake. Tatizo ni kwamba kanisa limepoteza walengwa wake.” Mwingine naye akasema, “Roho Mtakatifu hawezi kuwaokoa watakatifu na viti – lakini Kanisa limejaa vyote!”

Fikiri mfano wa kimatibabu. Tuseme kwamba Wizara ya Afya inaogopa kwamba kutatokea mlipuko wa surua. Ingefanya nini ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo? Bila shaka ingewatenga wenye ugonjwa huo na kuwaweka karantini wote ambao wamekwisha upata, na kwa njia hiyo ugonjwa ungezuilika. Sasa hebu fikiri – Wizara ya Jehanamu itake kuzuia mlipuko wa Ukristo wa Agano Jipya. Bila shaka ingefanya kila liwezekanalo kuwatenga “wabebaji” na kwa njia hiyo kuzuia kuenea kwake. Na hicho ndicho kinachotokea Kanisani kwa sehemu kubwa. Tunakaa ndani ya Kanisa kwa “mkao mtakatifu”. Timu yetu haiendi uwanjani, mahali ambapo ili kupata ushindi mchezo lazima ufanyikie. Na kuna wanaopenda mpango huu na uzuri wake na usalama wake. Maana, umewahi kumsikia mchezaji aliyeumizwa akiwa hajaingia uwanjani? Kwa hiyo, tunapanga mikakati yetu, tunafanya uchambuzi kuhusu adui yetu, tunarudiarudia mambo na hata kulaumu wachezaji wenzetu. Tunawaza kuhusu uanachama, mipango yetu, majengo na fedha. Kila juma tunakuwa na “gwaride” na amri yetu kuu ni “tubaki kama tulivyo”. Nimechanganya mifano hapo, lakini nadhani ujumbe umefika. Daima tunaongeza shughuli zetu za kidini, tunakamilisha mipango yetu kishirika, tunapanua na kukuza taasisi zetu za kidini, na kuimarisha taratibu zetu kiuongozi katika dini, na yote tunayofanya katika makanisa mengi ni kudumisha kawaida na kujistarehesha sisi wenyewe tu! Bila shaka Shetani anafurahi sana! Kanisa la kawaida linafanya kazi kwa kufuata mpango mbadala wa Shetani, badala ya kufuata mkakati wa Mwokozi.

3. KUPANUA MAONO

Sehemu ya tatu katika Agizo la Bwana wetu ni kuendelea kupanua maono. Upana wa eneo letu la utendaji katika Agizo hili ni “mataifa yote”.

Mkakati Wa Mwokozi

Hebu tujikumbushe tena – Yesu Kristo hafanyi mchezo nasi. Anatutazamia kabisa “tukabiliane” na dunia nzima! Naye ametupa Mpango ambao kwa huo tunaweza kufanikiwa! Je Mkristo – ni nia yako kugusa mataifa yote kwa “kuwageuza watu kuwa wanafunzi”? Hiyo kazi kuu ndiyo agizo la Bwana wetu. Kugusa dunia ndiyo utume wetu. Lengo letu lazima liwe kujulisha na kugusa dunia nzima mpaka mwisho wa nchi, mpaka ukamilifu wa dahari.

Hii hoja ya tatu katika Agizo inawezekana kuwa ndiyo ya maana kuliko zote. Hapa ndipo motisha kwa ajili ya kuwafanya watu kuwa wanafunzi inapotokea. Ningependa kutumia nafasi zaidi hapa ili kuhakikisha kwamba sote tunatambua ukuu wa Agizo la kuigusa dunia nzima. Dakta D. Martyn Lloyd-Jones alisema hivi katika kitabu chake kiitwacho The Miracle of Grace, “Sitasita kusema kwamba hatimaye, hakuna kipimo kamili cha ukiri wetu binafsi wa imani kama hali tuliyo nayo moyoni juu ya shughuli ya umisheni ya Kanisa.” Mimi niongeze maneno yangu hapa kwamba, “shughuli ya umisheni ya Kanisa” si kutuma waamini wenye mzigo maalum kwenda nchi za mbali tu. Huanza katika moyo wa kila aaminiye, na hutekelezwa kwa kila aaminiye kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo anayetambua kuhusu dunia nzima, anayelemewa na dunia nzima, anayeona dunia nzima, na mwenye kuwajenga na kuwaongeza wanafunzi wengine wenye kuiona dunia nzima na kuigusa dunia nzima.

Je, maono yako binafsi ni maono “makubwa kama ya Mungu”? Je, unakusudia kufika wapi na kugusa watu? Kipimo cha kufanikiwa kwako kama mwanafunzi wa Kristo kunaweza kuonekana katika jinsi unavyojibu maswali haya: Je, ushawishi ulio nao unafika mbali kiasi gani? Je, nini ukubwa wa eneo lako la uwezo? Isaya 54:2 inasema, “Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze. Ongeza urefu wa kamba zako, vikaze vigingi vya hema yako.” Mstari huu unatoa kauli mbiu kamili kabisa kwa ajili ya wote wanaofanya wengine kuwa wanafunzi (yaani, wanafunzi wote wa kweli wa Kristo), na hutoa mwito kwa ajili ya kukuza maono kusikokoma kwa kila aaminiye, ili kuigusa dunia nzima.

Hapa tena naomba ukabiliane na swali hili: Je, nini ukubwa wa eneo lako la uwezo na ushawishi? Je, unatenda kazi chini ya maono kama kofia, ambapo maisha ya Kikristo yanaanza na kuishia kwa ajili ya manufaa yako binafsi – ili uishi na upate kitu? Au je, maono yako ni kama mwavuli, yenye nafasi kwa ajili ya watu wawili au watatu hivi? Au je, maono yako ni kama kibanda cha simu, yenye nafasi ya kufunika watu kati ya watu hadi wanne? Au je, ni kama chumba, yenye kuwaingiza marafiki kadhaa? Au pengine yako kama nyumba, yenye uwezo wa watu kama 25 hadi 50 hivi? Au ni kama duka kubwa, yenye uwezo wa watu mia kadhaa, na hata elfu kadhaa? Au ni kama uwanja wa michezo, yaliyo na upana wa kutosheleza makumi elfu? Au pengine unatamani kuwa na maono kama anga, ambayo yanaweza kuwahusisha watu wote duniani na vizazi vyote vitakavyokuja? Kumbuka kwamba Agizo linahitaji maono yanayolingana na Yesu, yenye ukubwa wa Mungu, nasi tunatakiwa tuzidi kufanana na Kristo, kwa hali hiyo kuendeleza Tabia ya Mungu Mwenyewe. Tunakuwa “washiriki wa asili Yake ya Uungu” (ktk 2Petro 1:4) tunapo-okoka, na sehemu inayobaki ya maisha yetu inapaswa kutumika katika kushirikiana na kupanuliwa kwa Asili Yake ndani yetu. “Yeye hana budi kuzidi, bali mimi nipungue” (ktk Yohana 3:30). Sehemu ya huku kupanuka inamaanisha kuongezeka katika kujitambulisha na “Kinachomsumbua” Mungu – kumjulisha na kugusa kila mtu duniani kwa Ujumbe wa Injili Tukufu ya Kristo.

Ni dhahiri kutokana na kusoma Injili hata kwa juu juu tu kwamba, Yesu alikuja ili kuvamia, kufahamisha na kugusa dunia nzima. Angeweza kusema, “Mimi ni nuru ya Galilaya”, lakini hakufanya hivyo. Alisema, “Mimi ni nuru ya dunia” (ktk Yohana 8:12). Hakusema, “Mimi ni nuru ya Wabaptisti au WaPresbiterian au WaMethodisti”. Hakusema, “Mimi ni nuru ya waliolelewa vema au waliosoma vizuri au waliolishwa vizuri”. Angeweza kusema, “Mungu aliwapenda sana Wayahudi” lakini hakufanya hivyo. Alisema, “Mungu aliipenda sana dunia” (ktk Yohana 3:16). Yesu alikazia tena na tena kwamba hakuwa na mpango wa kufikia kisehemu kidogo au watu wachache – mpango Wake ulikuwa ni dunia nzima. Yeye ndiye nuru pekee ya kiroho kwa ajili ya kila nchi na kwa ajili ya kila mtu aliyeko katika kila nchi duniani.

Inasemekana kwamba askari wa jeshi la Napoleon walikuwa wanabeba ramani ya dunia katika mikoba yao, pamoja na bendera ya Ufaransa. Walikuwa ni wafungwa, mateka, watumwa wa wazo la kuiteka dunia kwa ajili ya Ufaransa. Enyi ndugu zangu Wakristo na dada zangu – Bwana wetu Mwenyezi ameweka maono yanayowaka ya dunia nzima mbele ya macho ya watu Wake na amewaomba kila mmoja kuyaruhusu yawake mpaka yachome moyo. Na haya maono yanapaswa kushika mawazo yetu kila wakati, mipango yetu, ndoto zetu, shughuli zetu kwa muda wote tunaoshi. Mara maono yatakapoanza kutushika, tutatambua kwamba Yesu aliweka mpango kwa ajili yetu – wewe na mimi kama watu binafsi – ili kutekeleza na kukamilisha maono yenyewe. Kufanya wanafunzi wenye maono ndiyo hilo! Unalionaje hilo?

Hebu tafakari swali hili kwa moyo wako wote. Je, Biblia na Ukristo vilitokea katika jimbo mojawapo kati ya majimbo hamsini ya Marekani? Hapana. Ukristo uliingizwa Marekani. Yesu hakuzaliwa nyumba ya jirani na kwetu, wala katika mtaa wetu. Biblia haikuwa imeandikwa kwa Kiingereza au Kiswahili tangu mwanzo. Sisi Wakristo wa Tanzania (au wa Afrika) ni matokeo ya wamishenari Wakristo. Je, na sisi tumejitoa kufanya katika sehemu zingine za dunia yale ambayo hawa wamishenari walitutendea sisi? Kama ungekuwa mmojawapo wa waliopotea katika Bara la Asia, Afrika au Marekani ya Latin, ungetamani mtu akuletee ujumbe wa Nuru na Uzima? Hakika sisi Wakristo wenye ubinafsi na wenye kujali zaidi taasisi na “makanisa ya kujikimu” lazima tutubu hasa na kuomba huruma na msamaha wa Bwana wetu, kwa sababu tumejaribu kumfanya Yeye kuwa mali yetu (kama Wayahudi walivyofanya) badala ya kuruhusu atutawale na kutumiliki kabisa. Na toba yetu lazima iwe ya kiwango cha ndani sana kiasi cha kufikia mahali pa kusahihisha hii hali ya “Ukristo wa kibinadamu” (neno langu, ambalo hata hivyo linapingana katika maana yake).

Ndugu John Oxenham katika kitabu chake kiitwacho Bees in Amber, aliandika hivi:

Nasikia sauti dhahiri kabisa ikiita, ikiita,

Inaita wakati wa usiku, hivi:

Enyi mnaoishi katika Nuru ya Uzima,

Tuleteeni na sisi hiyo nuru!

Tumefungwa katika minyororo ya giza,

Macho yetu hayapati kuona,

Enyi ambao hamjawahi kufungwa wala kuwa vipofu,

Tuleteeni nuru!

Haiwezekani – hamwezi kutusahau,

Sisi tulioko katika usiku wa giza kuu zaidi,

Sisi ni watu tunaozama, sisi ni watu tunaokufa,

Tuleteeni – Jamani, tuleteeni Nuru!

Sasa Mkristo, usije ukaanza kutafuta maandiko ya kunipinga au ya kuthibitisha kwamba watu pasipo Mungu wamekufa na hawawezi kusema hivyo! Najua hayo yote – amini hivyo! Hivyo sivyo watu wasiomcha Mungu wanavyoishi, wanavyofikiri au wanavyozungumza – lakini, ndivyo kila aaminiye anavyotakiwa kufikiri! Hatuwezi kuwaeleza watu waliokufa habari za kifo, wala hatuwezi kutazamia dalili za uhai, matendo na maneno kutoka kwao. Wala hatupaswi kuwatazamia wao kufufuka toka kwa wafu pasipo kuisikia sauti inayofufua wafu! Warumi 10 inaweka wazi kabisa kwamba, hakuna tangazo kwa waliopotea pasipo waliotumwa ili kutangaza ujumbe. Hakuna kusikia bila tangazo, hakuna imani pasipo kusikia, na hakuna wokovu pasipo imani (ktk Warumi 10:12-17)! Katika uhalisi, mambo yanaanzia wapi? Kwenye kutuma na kwenye kusema! Je, kanisa lenu liko katika shughuli ya kutuma? Je, linatumia fedha ili kutuma ili ujumbe uweze kusemwa? Uchaguzi pekee ni kutokutii amri ya Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana. Je, tutajisikiaje na tutafikiri nini tutakapohudhuria mbele ya Kiti cha Hukumu cha Kristo kama tulitumia huduma zetu tukikazia wale “Nyuki Wanaoua” – majengo, bajeti, miili, vipeperushi, majigambo, na kadhalika?

Kabla ya karne iliyopita kufika katikati, Charles Kingsley alitembelea visiwa vya New Hebrides huko Bahari ya Pacific ya Kusini na kushangazwa na ukatili na ulaji watu vilivyokuwepo. Aliporudi Uingereza aliandika makala kali iliyosema kwamba serikali ya Uingereza ingefanya huduma muhimu sana kwa binadamu kama wangetuma merikebu ya vita ili kuwaangamiza hao “washenzi” waishie baharini kama nzi wasumbufu, kwa kuwa hawakuwa binadamu na hakuna kitu ambacho kingeweza kufanyika ili kuwainua kutoka kiwango walichokuwa nacho.

Lakini, walikuwepo watu wengine ambao hawakukubaliana kabisa na tathmini ya Kingsley. Miongoni mwao alikuwepo Mkristo aliyempenda Mungu sana, jina lake John Paton kutoka Dumfries, Uskochi. Paton aliamini kwamba Injili ya Yesu ni nguvu ya Mungu iletayo wokovu (ktk Warumi 1:16), na kwamba Injili ina nguvu za kuhuisha, kuwafufua wale waliokufa katika dhambi (ktk Waefeso 2:1). Baada ya safari ndefu, Paton alifika kisiwa cha Tana huko New Hebrides, na akiwa hatarini daima ya kuuawa, alimhubiri Kristo kwa hao watu. Namwalika msomaji yeyote mwenye mashaka afanye utafiti wa matokeo yeye mwenyewe. Paton alipokufa, wenyeji wa kule walitengeneza kumbukumbu juu ya kaburi yake, iliyokuwa imeandikwa hivi: “Alipokuja, hapakuwa na nuru. Alipokufa, hapakuwa na giza”. Wapendwa – leo hii tunaweza kupenyeza kwa urahisi katika dunia nzima, kwa gharama ndogo kabisa na matatizo madogo tu ya usafiri. “Tumeketi” juu ya rasilmali kubwa sana ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kuwainjilisha na kuwafanya wengi sana kuwa wanafunzi hapa duniani. Maelfu ya Wakristo, makanisa, na watu waliopotea wangekaribisha na kuitikia upendo wetu katika nchi za karibu na mbali, nasi mara nyingi tunaketi tu katika hali ya kujidanganya katika makanisa yaliyokufa na yanayokufa mahali tulipo. “Mahali ambapo hakuna maono, watu huangamia.”

Siku ile ile Bandari ya Pearl Harbor iliposhambuliwa na madege ya kivita ya Japani, mishenari aliyerudi kutoka Mashariki ya Mbali alikutana na rafiki yake ambaye alikuwa hamwungi mkono katika anachofanya, naye akimtazama kwa jicho la kejeli na kuzungumza kwa sauti ya dharau alisema, “Ehe! Unasemaje kuhusu WaJapani wako sasa?” Yule mishenari akamjibu kwa upole na utaratibu, na kwa ujasiri kabisa, kana kwamba anamchoma upanga, “Nashukuru. WaJapani wangu hawajambo, wametulia katika neema ya Mungu. Kama unazungumza juu ya wale waliopiga mabomu meli za KiMarekani, hao ni WaJapani wako – wale ambao